Mechi za mwisho za kundi A Fainali za Ligi ya Mabingwa wa Mikoa (RCL) zimepigwa leo kwenye Viwanja tofauti katika muda mmoja.
Uwanja wa Halmashauri Bariadi kulikuwa na mchezo kati ya timu ya Bariadi United FC ya Simiyu ambayo imetoka sare ya kufungana mabao 2-2 na DTB FC ya Dar es Salaam.
Mchezo huo ulisimamiwa na Kamishna, Ibrahim Kidiwa kutoka Tanga, Muamuzi wa katikati Abel William kutoka Arusha, Muamuzi msaidizi namba moja Felix Sostenes wa Mbeya, Muamuzi msaidizi namba mbili Sikudhani Mkurungwa kutoka Njombe na Muamuzi wa akiba Ahmed Arajiga wa Manyara.
Dakika ya 19 Shomari Khalfan aliipatia bao la kwanza DTB FC,kabla ya dakika ya 31 Bariadi United kusawazisha kupitia kwa winga wao Enock Enock akiunganisha mpira wa kona iliyopigwa na Baraka Magesa, mabao ambayo yalidumu mpaka mwisho mapumziko.
Dakika ya 51 kipindi cha pili Iddi Zungo alipatia DTB FC bao la pili baada ya kona iliyopigwa na Ally Dilunga
Bariadi walipata bao la kusawazisha dakika ya 66 kwa mkwaju wa penati baada ya golikipa wa DTB FC kumshika mshambuliaji wa Bariadi United eneo la hatari penati iliyofungwa na Gilbert Boniface matokeo yaliyodumu mpaka mwisho wa mchezo.
Mchezo wa pili umechezwa kwenye Uwanja wa Bariadi Sekondari ukiwakutanisha Top Boys FC ya Ruvuma na Isanga Rangers FC ya Mbeya, ukisimamiwa na Kamishna, Judith Gamba kutoka Dodoma, Muamuzi wa katikati Amina Kyando wa Morogoro, Muamuzi msaidizi namba moja Ramadhani Kiloko wa Tanga, Muamuzi msaidizi namba mbili Sadi Salum wa Kigoma na Muamuzi wa akiba Tatu Malogo wa Tanga
Mchezo huo umemalizika kwa timu hizo kutoka sare ya kufungana bao 1-1
Bao la Top Boys FC likifungwa dakika ya 43 na Isanga Rangers FC wakichomoa dakika ya 55.
Kwa matokeo ya michezo hiyo timu ya Isanga Rangers FC na Bariadi United zimesonga hatua ya nusu fainali.
Kesho fainali hizo zinaendelea kwa michezo miwili, itakayochezwa katika Viwanja viwili tofauti Uwanja wa Halmashauri Pan African FC na Mji Mpwapwa FC na Uwanja wa shule ya Sekondari ya Bariadi Mbuni FC na Mkurungezi FC,michezo itakayochezwa katika muda mmoja