Semina ya Waamuzi wa Fifa na Elite Yahitimishwa.

Makamu wa pili wa Rais wa TFF Steven Mnguto amehitimisha rasmi semina ya siku tano ya waamuzi wa FIFA na Elite leo Julai 29, 2022 katika uwanja wa Benjamini Mkapa jijini Dar es Salaam.

Semina hiyo yenye mjumuisho wa waamuzi 34 kutoka Tanzania Bara na visiwani ilikuwa na lengo la kuwajengea waamuzi uwezo zaidi wa kutafsiri sheria za mpira wa miguu na kuweka miili yao katika hali ya utimamu .

Akizungumza wakati wa kufunga semina hiyo makamu wa pili wa TFF Steven Mnguto aliwapongeza waamuzi kwa kuonesha utayari wa kutaka kujifunza mambo mapya na kuwataka waamuzi kuzingatia yote waliyojifunza kutoka kwa wakufunzi wao ili kukuza mpira wa miguu Tanzania.

“Tunawataka waamuzi mkatafsiri sheria 17 za mpira wa miguu vile inavyotakiwa na kuhakikisha mpira wa miguu unakuwa mchezo wa kiungwana kwa pande zote mbili kwani msimu mpya utakaoanza mwezi Agosti utakuwa mgumu na wa ushindani kutokana na timu zote kufanya usajili mzuri pamoja na maboresho mengi kwa timu zote; hivyo waamuzi mkawe sehemu ya kuifanya ligi yetu iwe bora na yenye kuvutia ili hata wadhamini wazidi kuongezeka.”

Naye mkufunzi wa semina hiyo Jason Demoo alisema anaushukuru uongozi wa TFF kwa mapokezi mazuri na kwa kuandaa semina hiyo kwani imekuwa msaada mkubwa kwa waamuzi kujifunza. Alieleza kuwa viwango vya wamuzi kwa mwaka huu vimekuwa bora zaidi ya mwaka uliopita na waamuzi wote wamefaulu mtihani wa utimamu wa mwili na ule wa nadharia.

Waamuzi walioshiriki katika semina ni Helly Ally Sassi, Ramdhani Kayoko, Ahmed Arajiga, Nasir Siyah, Fiorebtina Zablon, Tatu Malogo, Ferdinand Chacha, Mohamed Mkono, Frank Komba, Soudi Iddi, Kassim Mpanga, Ally Rajabu, Hellen Mduma, Janeth Balama, Glory Tesha, Emmanuel Mwandembwa, Hance Mabena na Abdallah Mwinyimkuu

Wengine ni Raphael Ikambi, Joachim Akamba, Gilbert Mrina, Mohamed Khamis, Hamdani Said, Leonard Mkumbo, Black Tubuke, Sharif Mohamed, Yusuph Dadi, Ally Mbwana, Jonesia Kabakama, Amina Samwel, Ester Adabert, Zawadi Yusuph na Sikudhani Mkurungwa.