Semina ya Wakufunzi wa Waamuzi Yafunguliwa Rasmi Dar

Semina maalumu ya kuwaandaa wakufunzi watakao tumika kutoa mafunzo kwa waamuzi imefunguliwa rasmi Novemba 06, 2023 Dar es Salaam na Mwenyekiti wa mashindano Tanzania ambaye pia ni mjumbe wa Kamati tendaji TFF Khalid Abdallah.

Kozi hiyo ya siku tano itakayo jikita zaidi kwenye maeneo ya utimamu wa mwili na kiufundi imejumuisha washiriki 49 kutoka mikoa mbalimbali Tanzania bara na visiwani watakao patiwa mafunzo hayo na wakufunzi wa CAF Maroua Hannachi kutoka Tunisia atakaye jikita kwenye eneo la utimamu wa mwili akishirikiana na Carlos Manuel Neves kutoka nchini Afrika Kusini atakaye jikita kwenye eneo la kiufundi.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa semina Mwenyekiti wa mashindano Tanzania Khalid Abdallah amewataka washiriki hao wakajitoe kwa kuifanyia kazi taaluma yao kwa lengo la kusongesha zaidi gurudumu la mpira wa miguu hapa kwetu Tanzania na hata Duniani.

“Tutumieni nafasi hii kwenda kupeleka elimu kwenye mikoa yetu ili tuzalishe vijana wengine wengi zaidi, pia nashukuru hapa kuna vijana tumetoka nao kwenye mashindano ya RCL lakini hii leo wanachezesha mechi kubwa za ligi kuu hivyo nataka iwe hivi na zaidi kwaajili ya Shirikisho letu” alisema Khalid

Kwa upande wa mkufunzi Carlos Manuel Neves kwa niaba ya wakufunzi wengine aliwataka washiriki wawapatie ushirikiano kwa muda huo wa siku tano, huku akisisitiza kuwa hilo ndilo jambo pekee litakalo fanikisha malengo waliyonayo ya kusongesha mpira wa miguu kwa upande wa waamuzi hata kufikia ngazi za juu zaidi Afrika na duniani.