Serengeti Boys kushiriki mashindano ya Aegean 2022.
Kikosi cha timu ya Taifa ya vijana wenye umri chini ya miaka 17 (U-17) Serengeti Boys kimeingia kambini tayari kujinoa na mashindano ya Aegean 2022 (Aeagen Cup Tournament), yanayotarajia kuanza kurindima Januari 15 huko nchini Uturuki.
Kikosi hiko kinachojumuisha wachezaji 30 kutoka mikoa mbalimbali kilipatikana baada ya mchujo wa Zaidi ya mara tatu kwa kucheza mechi na timu tofauti ili kupima uwezo wa wachezaji wenye viwango ambao mwishoni walipata nafasi ya kuunda kikosi hiko.
Akizungumza baada ya kumaliza mazoezi katika uwanja wa Karume kocha mkuu wa Serengeti Boys Maalim Saleh alisema, mwaka huu wamepata wachezaji wengi wenye vipaji vya hali ya juu ukilinganisha na miaka mingine iliyopita, lakini pamoja na vipaji vyao bado kuna kazi kubwa ya kuwatengeneza na kuwaongezea baadhi ya mbinu ili wawe katika hali ya utayari wa mashindano hasa ukizingatia wengi ni wageni na hawana uzoefu katika mashindano ya kimataifa.
“ Mashindano ya Aegean sio mepesi kwa kuwa yanajumuisha timu nyingi bora kutoka mabara tofauti tofauti huku zikiwa zimesheheni upeo mkubwa na wachezaji wake wamepata mafunzo na wamekuzwa katika misingi ya soka hivyo ninaona kabisa ushindani utakuwa mkubwa jambo ambalo kwa upande wangu nitahakikisha mambo yote ya kiufundi na mbinu za kiushindani zinafundishwa na kueleweka kwa wachezaji ndani ya siku 10 ambazo watakaa kambini kabla ya kuianza safari ya Uturuki” alisema Maalim.
Hii itakuwa ni mara ya tatu kwa Serengeti boys kushiriki mashindano hayo ambapo kwa mara ya mwisho walishiriki mwaka 2020 na kuibuka kuwa washindi wa tatu wakitoka sare na mwenyeji timu ya Uturuki, huku mwaka 2021 mashindano yakishindwa kufanyika kutokana na kuibuka kwa ugonjwa wa Uviko -19.