Timu ya Tanzania ya vijana wasiozidi umri wa miaka 17 ndio mabingwa wa Kombe la Vijana la mataifa ya Afrika Mashariki na Kati Cecafa wa mwaka 2017.

Serengeti Boys walitwaa ubingwa baada ya kuwalaza Somalia mabao 2-0 katika mechi ya fainali iliyochezewa mjini Bujumbura, Burundi.

Mabao ya Serengeti yalitiwa kimiani na Edson Jeremiah na Japhary Mtoo.

Ushindi huo ndio wa kwanza tangu kuanzishwa kwa michuano hiyo mwaka 2007 na unatarajiwa kuwatia moyo vijana hao wanapijiandaa kushindi michuano ya Kombe la Vijana Mabingwa Afrika mwaka 2019.

Serengeti Boys walianzisha kampeni yao baada ya kutoka sare 1-1 na Uganda mechi yao ya kwanza lakini mechi ya pili wakalaza Sudan 6-0 uwanja wa Muyinga mjini Bujumbura.

Nusufainali, Serengeti walipata ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Kenya katika mchezo uliopigwa katika uwanja wa Muyinga.

Somalia walifika fainali kwa kulaza Kenya 1-0 katika moja ya mechi zao za hatua ya makundi.

Zanzibar walidaiwa kuwasilisha wachezaji 12 wasiohitimu kucheza na wakaondolewa kwenye michuano hiyo na kutozwa faini ya Sh1.5 milioni.