Serengeti Girls Miongoni mwa timu 16 Zilizo fuzu Kombe la Dunia

Timu ya Taifa ya wasichana wenye umri chini ya  miaka 17 Serengeti Girls rasmi imeweza kufuzu kushiriki Fainali za Kombe la Dunia baada ya ushindi wa bao 1-0 kwenye mchezo wao dhidi ya Cameroon Juni 05, 2022 kwenye uwanja wa Amaan huko visiwani Zanzibar.

Serengeti Girls imeweza kufuzu katika hatua hiyo kwa jumla ya ushindi wa mabao 5-1 baada kuichabanga Cameroon kwenye mchezo wa ugenini kwa mabao 4-1 wiki mbili zilizo pita, na kumaliza hesabu hizo nyumbani kwa bao moja pekee lililo ifanikisha kuisindikiza timu hiyo kibabe kwenye fainali hizo zinazo tarajiwa kupigwa nchini India Oktoba mwaka huu.

Hata hivyo kikosi hicho kiliwasili uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere usiku wa Juni 05,2022 majira ya saa 3 usiku  ikitokea Zanzibar kwenye mchezo wao wa hatua ya tatu dhidi ya Cameroon. Serengeti Girls pia ndio timu iliyotoa kinara wa ufungaji wa magoli Clara Luvanga mwenye jumla ya magoli 10.

Kufuatia ushindi huo na uwakilishi wa kipekee wa Taifa uliofanywa na timu hiyo, serikali kupitia wizara ya Utamaduni ,Sanaa na Michezo iliweza kuipatia mwaliko timu hiyo kujumuika Bungeni mapema asubuhi ya leo wakati wizara ikiwasilisha bajeti yake iliyosomwa na Mhe. Waziri Mohammed Mchengerwa.

Ikumbukwe Serengeti Girls imekuwa ni miongoni mwa timu chache kutoka Bara la Afrika kwenda kuwakilisha mataifa mengine kwenye michuano hiyo, hata hivyo mafanikio hayo ni kutokana na juhudi endelevu za takribani miaka 4 zilizofanywa na uongozi wa Shirikisho la Mpira wa Miguu TFF chini ya uongozi wa Rais Wallace Karia na Katibu wake Kidao Wilfred kushirikiana na juhudi za kiufundi za kocha mkuu wa timu hizo za Taifa kwa wasichana Bakari Shime sambamba na benchi lote la Ufundi.