Serengeti Girls ni Swala la Muda

Timu ya Taifa ya wanawake U17 “Serengeti Girls ” iliyokambini kujiandaa na mchezo wa kufuzu kombe la Dunia dhidi ya timu ya Taifa ya Zambia unaotarajiwa kuchezwa Februari 3, 2024 imeendelea na mazoezi ya utimamu wa mwili ilihali kujiweka sawa katika kuzichanga karata zake vyema kabla ya kuuendea mchezo wake huo.

Ikumbukwe timu ya Serengeti Girls iliwahi kushiriki michuano hiyo mwaka 2022 huku ikiacha rekodi ya kuwa timu ya kwanza Tanzania kufika mpaka hatua ya robo fainali, hivyo itauendea mchezo huo huku ikiwa na kumbukumbu nzuri katika mechi zake za hatua kama hiyo.

Akizungumzia maandalizi na maendeleo ya kambi kwa ujumla kocha wa utimamu wa mwili Elieneza Nsanganzelu alisema wanaendelea kuwapatia baadhi ya mazoezi wachezaji hasa yale ya kuwaweka sawa kimwili na kakili, huku wakitazamia muda sahihi wa kuanza mazoezi ya kimbinu zaidi.

“Tumekuwa na vipindi tofauti tangu tumeingia kambini, nafurahi kuona wasichana wanapokea vizuri maelekezo tunayowapatia, hivyo tunatarajia kuwaongezea zaidi baadhi ya mbinu hasa zitakazo tusaidia kwenye mchezo wetu wa awali ugenini ” Alisema Elieneza

Serengeti Girls inatarajia kuanza ugenini Zambia kabla ya kurudiana Februari 11 hapa nyumbani katika uwanja wa Azam Complex Chamazi.