Serengeti Girls Yabeba Ubingwa UNAF
Timu ya Taifa ya wasichana U17 “Serengeti Girls” iliyokuwa inashiriki mashindano ya mataifa ukanda wa kaskazini Kwa wasichana U17 UNAF, imefanikiwa kuipeperusha vyema bendera ya Taifa baada ya kutwaa Ubingwa wa mashindano hayo.
Serengeti Girls imetwaa Ubingwa huo baada ya kutoka sare na timu mwenyeji “Tunisia” kwenye mchezo wa mwisho uliopigwa Septemba 7, 2024 uwanja wa Ariana na Tanzania kutwaa Ubingwa huo kwa faida ya tofauti ya magoli mengi zaidi.
Ikiwa kwenye mashindano hayo Serengeti Girls ilifanikiwa kufunga jumla ya magoli 9 na kuruhusu magoli 4, tofauti ya magoli 2 na timu ya Tunisia iliyoshika nafasi ya pili kwa faida ya magoli 3.
Tanzania ilipata ushindi wa magoli 4-1 dhidi ya Misri kwenye mchezo wa kwanza, na baadae ikabeba alama tatu nyingine mbele ya Morocco kwa matokeo ya Tanzania kushinda magoli 5-3. Wakati Tunisia waliomalizana Kwa suluhu ya bila kufungana wenyewe walishinda 2-0 dhidi ya Morocco na baadae wakashinda kwa magoli 2-1 dhidi ya Misri.
Hata hivyo kwa matokeo hayo Tanzania inaendelea kuweka rekodi nzuri na bora zaidi kwenye ukanda huo baada ya Serengeti Girls kufikia rekodi waliyoacha dada zao ya kubeba ubingwa hivi karibuni kwenye mashindano ya Tunis Women’s Cup yaliyofanyika nchini humo.