Serengeti Girls Yatakata Ugenini

Timu ya wasichana chini ya umri wa miaka 17, Serengeti Girls imefanikiwa kuibuka na ushindi mnono dhidi ya Burundi baada ya kuiadhibu kwa jumla ya mabao 4-0 katika mchezo uliochezwa kwenye uwanja wa Urukundo Mjini Ngozi, Aprili 16, 2022.

Mchezo huo ulianza kwa timu zote kushambuliana kwa zamu huku Burundi wao wakionekana kuutaka ushindi kwa nguvu; wakifanya kosakosa za hapa na pale kwenye dakika 20 za kwanza.

Tanzania iliamka mnamo dakika ya 25 na kupeleka mashambulizi makali yaliyosababisha kupata kona uliyochongwa na Veronica Mapunda na kumkuta Clara Luvanga aliyepachika mpira huo kimiani dakika ya 32; bao lilodumu mpaka timu hizo zinakwenda mapumziko.

Kipindi cha pili kilianza kwa kasi kama kawaida Burundi walikuwa wa moto zaidi baada ya kupeleka mashambulizi makali kwenye lango la Serengeti Girls; hata hivyo, safu ya ulinzi ya Tanzania iliyazimisha mashambulizi hayo kwa kufanya shambulizi la kushtukiza lilozaa bao la pili lilofungwa na Neema Kinega kunako dakika ya 53.

Msumari wa tatu ulikomelewa na Clara Luvanga dakika ya 81 kabla ya Husna Mpanja kushindilia nyavuni goli la 4 likifungwa katika dakika ya 88 na kuhitimisha mchezo huo kwa kuifanya Serengeti Girls kuibuka na ushindi mnono wa bao 4-0.

Badaa ya mchezo huo kocha Mkuu Bakari Shime alisema kuwa matokeo waliyoyapata yanatokana na maandalizi mazuri ya timu na sapoti ya TFF, Serikali inayoongwa na Rais Samia Suluhu Hassan pamoja na wadau mbalimbali waliojitokeza kuitia moyo timu hiyo.

Shime aliongeza akisema bado malengo yya timu hayajiafikiwa hivyo ushindi walioupata ni deni kubwa kwa mchezo wa pili utakaochezwa Mei Mosi Mjini Zanzibar mwaka huu. Kwa upande wa kocha wa Burundi yeye hakupata fursa ya kuongea na vyombo vya habari baada ya mchezo.

Naye Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Pauline Gikul alisema kuwa ameyapoke matokeo hayo kwa furaha kubwa na atakwenda kupeleka salamu kwa Rais jinsi alivyoshuhudia jitahada za wasichana hao katika mchezo huo. Wakati Balozi Jilly (Dkt) akiwapongeza na kuahidi kuendelea kutoa ushirikiano wake mpaka hapo timu itakapoondoka kurejea Dar es Salaam kwa ajili ya maandalizi ya mchezo wa pili.

Mchezo huo kati ya Serengeti Girls na Burundi ni wa kusaka nafasi ya kushiriki Kombe la Dunia nchini India, Oktoba mwaka huu, ulihudhuriwa na viongozi na wananchi wengi kutoka Bujumbura, Ngara na maeneo mengine yaliyo karibu na mipaka ya Burundi na Rwanda pia.

Baadhi ya viongozi waliohudhuria ni Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Pauline Gekul, Balozi Dkt. Jilly Maleko, Makamu wa Rais wa TFF Athuman Nyamlani, Rais wa ZFF, Abdullatif Said Yassin, Mkurungezi wa Mashindano wa TFF na viongozi wengine kutoka Ngara na Makao Makuu ya TFF.