Serikali yaikabidhi Serengeti Girls milioni 40

Serikali kupitia wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo imeizawadia timu ya Taifa ya wanawake U17 Serengeti Girls shilingi milioni 40 kwa kufanikiwa kufika hatua ya robo fainali kwenye Fainali za Kombe la Dunia India 2022.

Fedha hizo zimekabidhiwa na Waziri Mohammed Mchengerwa katika hafla fupi ya kuipokea Serengeti Girls iliyofanyika uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.

Waziri Mchengerwa alisema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mheshimiwa Samia Suluhu Hassan amefurahishwa na hatua ambayo timu hiyo imefika na amewapongeza kwa kazi kubwa waliyoifanya.

“Hongereni sana vijana mmepambana na mmelitangaza, taifa nawasihi msibweteke endeleeni kufanya mazoezi ili mzidi kuimarika kiafya na mzidi kuwa na uwezo wa kucheza vizuri katika mashindano mbalimbali yaliyo mbele yenu “ alisema Mchengerwa.

Hafla hiyo ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali na TFF wakiongizwa na Rais Wallace Karia.