Serikali kuipa Taifa Stars million 500 ikifuzu Afcon 2023

Serikali ya Jamhuri ya muungano wa Tanzania kupitia Waziri wa utamaduni sanaa na michezo Mheshimiwa Dkt. Pindi Hazara Chana imetoa ahadi ya kutoa shilingi milioni 500 Kwa timu ya taifa ya Tanzania Taifa Stars endapo itafanikiwa kufuzu AFCON  2023.

Akizungumza na waandishi wa habari  Waziri Chana alisema serikali  inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan imedhamiria na imejipanga kuleta mabadiliko na kuwekeza zaidi katika michezo ili Taifa liendelee kujitangaza kimataifa lakini pia kuendelea kuwaunga mkono na kuwapa morali wachezaji wanaojitoa kulipambania Taifa.

” Watanzania tuwe pamoja kuiombea nchi yetu tuna imani kubwa na uwezo walionao wachezaji wetu. Wakati umefika sasa wa Tanzania kuzidi kuingia kwenye ramani za kimataifa” alisema Waziri Chana.

Mbali na hayo Waziri huyo aliwatakia heri wachezaji wa Taifa stars kuelekea katika michezo miwili ya kufuzu AFCON  dhidi ya timu ya taifa ya Uganda na kuwataka mashabiki wajitokeze kwa wingi katika mchezo wa marudiano ambao utapigwa katika uwanja wa Benjamin Mkapa Machi 28, 2023.

Kikosi cha Taifa Stars chini ya kocha Adel Amorouche  tayari kipo nchini Misri kikiendelea kujinoa  kuelekea katika mchezo wa Kwanza dhidi ya Uganda ‘The Cranes’  siku ya Machi 24, 2023.