Serikali Yampongeza Rais Karia Kuipeleka Serengeti Girls Kombe la Dunia India  Oktoba, 2022

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imemmwagia sifa Rais wa Shirikisho la Mpira Tanzania (TFF) kwa kufanikisha kuipeleka Kombe la Dunia timu ya wasichana wenye umri chini ya miaka 17 itakayofanyika kuanzia Oktoba 11, 2022 nchini India.

Pongezi hizo zilitolewa na Waziri wa Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe. Mohammed Mchengerwa alipokuwa anato hotuba fupi kwenye hafla ya Usiku wa Mastaa wa Soka iliyofanyika katika Hoteli ya Johari Rotana iliyopo jijini Dar es Salaam Julai07, 2022.

Mhe. Mchengerwa alisema Rais Wallace Karia amekuwa ndiye kiongozi wa kwanza katika historia ya soka nchini kuipeleka timu ya Taifa ya Tanzania kwenye mashindano makubwa duniani kupitia timu ya mpira wa miguu ya wasichana wa U17 (Serengeti Girls).  Akitoa pongezi kwa Rais Karia, hakusita kumpa kongole Clara Luvanga kwa kuibuka mfungaji bora Afrika ambaye pia alishika nafasi ya pili duniani katika michezo ya kusaka kushiriki Kombe la Dunia kule India.

Alisema kuwa kazi iliyofanywa na TFF si ya lelemama ni kazi ambayo inapaswa kuenziwa na kuungwa mkono kwa hali na mali ili taifa liendelee kupeperusha vyema Bendera ya nchi kwa kuzipeleka timu nyingine nyingi katika michuano mbalimbali ya Afrika na Dunia pia.

Aidha, Waziri Mchengerwa aliongeza akisema katika kutambua juhudi za Rais Karia na viongozi wengine wa TFF, Serikali imeamua kuendelea kutenga bajeti kwa ajili ya ukarabati wa viwanja vya soka nchini huku ikiahidi kujenga viwanja vingine vipya. Aliongeza kuwa mafanikio hayo aliyoyafanya Rais Karia si madogo kwa Tanzania kwani anakumbuka hata yeye alipokabidhiwa Wizara hiyo alitoa ahadi ya kuhakikisha timu zinafika kombe la dunia na kwenye mashindano mengine ya Afrika kama AFCON; japokuwa hakubainisha ni timu ipi itakayoanza kufanya hivyo kwa vitendo.

Waziri Mchengerwa aliongeza kuwa mafanikio hayo yanachagizwa pia na ushirikiano wa Mhe. Rais wa Jumhuri wa Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan ambaye amekuwa karibu na Shirikisho na amekuwa akitoa maelekezo  kwenye Wizara pamoja na Baraza la Michezo la Taifa na taasisi zote zinazosimamia michezo kuhakikisha zinafuatilia na kutekeleza kwa vitendo maelekezo yake.

Aliendelea kueleza kuwa katika hatua za awali Serikali imekusudia kuanza kufanya ukarabati wa viwanja sita; CCM Kirumba Mwanza, Mkwakwani Tanga, Jamhuri Dodoma,  Sheikh Amri Abedi Arusha, Sokoine Mbeya na Amani Zanzibar huku  ikijipanga kufanya ukarabati mkubwa katika kiwanja cha Uhuru na marekebisho madogo kwenye uwanja wa Benjamin Mkapa yote ikiwa Dar es Salaam.

Mbali na ukarabati huo Waziri Mchengerwa alisema Serikali imekwisha panga kujenga Eneo la Michezo (Sports Arena) litakalo jengwa Tanganyika Packers Dar es Salaam.

Alisisitiza kuwa Serikali inayoongozwa na Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan tayari imekwisha kutenga bajeti ya ukarabati wa viwanja vilivyotajwa, pamoja na kujenga vingine vipya kimojawapo kikiwa kiwanja kikubwa kitakachojengwa Dodoma. Alisema zoezi hilo litakuwa ni endelevu kwenye mikoa mingine kadri bajeti ya Serikali itakavyoruhusu

Sambamba na hilo, Waziri aliwapongeza washindi wote wa TUZO tofautitofauti, waandaaji wa hafla hiyo (Kamati ya Utoaji Tuzo), wafanyakazi na wadau wote wa soka bila kuwasahau wadhamini wakuu wa Ligi Benki ya NBC, Azam Media Ltd., Shirika la Utangaji la TBC na Serengeti kwa uwekezaji mkubwa walioufanya ambao umeiwezesha ligi ya Tanzania kuwa miongoni mwa Ligi Bora Afrika.

Katika suala la maadili Waziri Mchengelewa alivieleza vyama vya mpira na taasisi zote zinazosimamia mpira wa miguu kuwa ni lazima vitilie mkazo wa hali ya juu kwenye suala la nidhamu na maadili ya wachezaji, viongozi wa klabu zinazoshiriki ligi mbalimbali na wadau wa soka ili kuweza kuweka taswira nzuri ya soka kitaifa na kimataifa pia.

Akitoa shukrani kwa Serikali, Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania Wallace Karia alisema wanamshukuru Mhe. Rais wa Jumhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan kwa ushirikiano wake kwao kama taasisi; kwani amekuwa na mchango mkubwa si tu kwa kufuta baadhi ya gharama za vifaa vya michezo bali pia kwa motisha anaowapatia wachezaji wa timu za taifa, pongezi kwa klabu zinazofanya vizuri na ushauri wenye kujenga na kuendeleza soka anaowapatia viongozi wa mpira kwa nyakati tofautitofauti.