Serikali yaongeza nguvu Taifa Stars.

Waziri Mkuu wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa ametoa rai kwa wadau na wapenzi wa soka kote nchini kuungana kwa pamoja na kuhakikisha timu ya soka ya taifa inafanya vizuri katika michezo miwili iliyobakia ya kuwania nafasi ya kushiriki Kombe la Dunia kwa mwaka 2022 nchini Qatar.

Mhe. Majaliwa aliyasema hayo baada ya ‘Taifa Stars’ kufanya vizuri katika kundi lake ambapo kwa sasa timu hiyo ndio kinara wa kundi J na ikiwa atashinda michezo yake miwili iliyobaki dhidi ya DR Congo na Madagascar,Taifa stars itaweka historia mpya ya kufuzu kushiriki Kombe la Dunia kwa mara ya kwanza tangu kupatikana kwa uhuru wa Tanzania.

Akizungumza wakati wa kikao cha pamoja kilichohusisha wadau mbali mbali wa soka nchini katika ukumbi uliopo uwanja wa Uhuru, jijini Dar es Salaam, Waziri mkuu alitoa wito huo ambapo kiasi cha sh. Bilioni 1.6 kilichangwa ili kuisaidia Taifa stars katika maandalizi ya mechi zilizobaki dhidi ya DR Congo na Madagascar.

Aidha, Mhe. Majaliwa alisema lengo la Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan ni kuhakikisha sekta ya michezo inakua na kufanya vizuri ndani na nje ya nchi. Katika kufanikisha lengo hilo Rais anataka kuona mikakati na mipango bora inawekwa kwenye Nyanja zote za michezo nchini ili wanamichezo wapeperushe vyema bendera ya Taifa katika mashindano ya kimataifa.

“Kikao hiki kimefanyika baada ya maelekezo ya Mh. Rais wetu wa jamuhuri ya muungano wa Tanzania ambaye ameonesha nia njema ya kuendeleza sekta ya michezo nchini ambapo ameonyesha kufurahishwa na mwenendo wa michezo nchini hasa mpira wa miguu na ana imani kwamba Taifa Stars iko kwenye nafasi nzuri ya kuipa heshima Tanzania kucheza kombe la dunia”Alisema Mhe. Majaliwa.

Kwa upande mwingine, Mhe. Majaliwa alitoa wito kwa wamiliki wa viwanda,watu binafsi na taasisi za umma kuendelea kujitokeza kuchangia timu ya Taifa ili iweze kuandika historia mpya kwa Tanzania kufuzu kushirki kombe la Dunia kwa mara ya kwanza tangu . Aliendelea kutoa hamasa kwa wananchi kuvaa jezi ya timu yetu ya taifa siku ya mechi hata kama hawatafika uwanjani na watakaopata nafasi ya kufika uwanjani kulingana na maelekezo ya CAF basi wafike kwa idadi hiyo kwa ajili ya kuishangilia timu yao.

Kikao hicho cha pampoja kilihudhuriwa na Rais wa TFF Wallace Karia, Katibu Mkuu wa TFF Kidao Wilfred na wadau kutoka makampuni na mashirika mbalimbali; baadhi ya wadau walioshiriki katika kikao hicho ni pamoja na Taifa Gas, CRDB, NBC, LAKE OIL, STAR OIL, K4 SECURITY, KAMBIASO, GSM na wengineo.