Shime Aanza Kuchanga Karata Zake Kombe la Dunia India

Jumla ya wachezaji 26 wanaounda timu ya Taifa ya wasichana chini ya miaka 17 wimeingia kambini huko visiwani Zanzibar kuiwinda Botswana kwenye mchezo wao wa awali unaotarajiwa kuchezwa Machi 06, 2022 ikiwa ni katika kuisaka tiketi ya kushiriki Kombe la Dunia mwezi Oktoba mwaka huu huko nchini India.

U17 ambao wamefunga safari hii leo kutokea Dar es Salaam tayari wamewasili Zanzibar wakiwa chini ya Kocha mkuu Bakari Shime, ambaye alisema kuwa wamepata uzoefu mkubwa wa mashindano ya aina hiyo mara baada ya kutoka kushiriki na timu ya Tanzanite ambayo ilifanikiwa kufika mpaka hatua ya nne kwenye mashindano ya kufuzu Kombe la Dunia nchini Costa Rica kabla ya kukwamishwa  na Ethiopia wakipoteza kwenye mchezo wa ugenini.

Shime alisema kikosi chake kipo tayari kwaajili ya mchezo kwani maandalizi walianza mapema tangu wakiwa kwenye mashindano waliyokuwa wakishiriki timu ya Tanzanite kutokana na kuwa asilimia kubwa ya timu ya Tanzanite inaundwa na wachezaji ambao wanachezea timu ya U17, hivyo kambi yao itakuwa ni kufanya maandalizi ya mwisho.

“tumejifunza mengi, tumefahamu sababu ambazo zilipelekea kushindwa kuendelea na mashindano na kufikia pale tulipokusudia kufika hivyo uzoefu huo ndio tutahakikisha tunakwenda nao kwa wakati huu ili kuweza kufikia malengo yetu ya timu ya U17. Tupo kwenye mchakato wa kutafuta maendeleo ya kweli ya mpira, na haijalishi ni wakati gani tutafikia hapo isipokuwa ni muhimu kufuata taratibu tulizojiwekea.” Kocha Bakari Shime

U17 wamewahi kushiriki mashindano kama hayo mwaka 2019-2020 ambapo waliishia kwenye hatua ya 3 mara baada ya  kupoteza kwenye mchezo wa ugenini dhidi ya Uganda , kabla ya mchezo huo walimtoa Burundi kwa kumfunga michezo yote miwili wakiwa ugenini na nyumbani.Hata hivyo mashindano hayo hayakuendelea mbele zaidi kutokuana na mlipuko wa ugonjwa wa Uviko 19.