Simba Azam Hakuna Mbabe Chamazi

Mechi tisa za ligi Kuu Bara zilizochezwa Julai 15, 2021 katika viwanja mbali mbali nchini imekuwa na chungu tamu kwa baadhi ya timu, huku timu nyingine zikiibuka na matokeo ya mabao lukuki na hivyo kufufua matumaini.

Michezo hiyo iliyokuwa ikikamilisha mzunguuko wa 33 kwa kila timu ya ligi hiyo ilionekana kufufua matumaini kwa baadhi ya timu huku timu nyingine zikizidi kudidimia chini zaidi kutokana na kasi ya mawimbi kulizidi jahazi na hivyo kupelekea kuzama.

Michezo hiyo tisa iliyochezwa ilizikutanisha timu zote za ligi Kuu Bara ambapo michezo ya mapema ilikuwa ni kati ya Biashara United na Tanzania Prisons waliotoka sare ya (1-1), KMC dhidi ya JKT Tanzania (5-2) na Ruvu Shooting dhidi ya Namungo (2-1) michezo hiyo yote ilichezwa majira ya 8:00 mchana.

Michezo migine ilichezwa saa 10:00 amabyo ilizikutanisha timu za Young Africans dhidi ya IHEFU FC, matokeo yalikuwa ni (2-0), Dodoma Jiji dhidi ya Mtibwa Sugar wakatoka sukuhu tasa(0-0), Mbeya City nao wakailaza Gwambina kwa bao 1-0, Polisi Tanzania wao walikubali kichapo cha bao moja kwa sifuri (0-1) dhidi ya Kagera Sugar huku Wagosi wa Kaya (Coastal Union) wa Tanga ikiwashushia kipigo kitakatifu cha bao 5-0 wachimba Almasi kutoka Shinyanga Mwadui FC katika uwanja wao wa Mkwakwani Tanga.

Mchezo wa saa kumi jioni kati ya Young Africans na IHEFU FC ulihusisha tukio la kumuaga kiungo wao raia wa Rwanda Haruna Niyonzima, Jezi (8) aliyeitumikia timu hiyo kwa miaka mingi na kwa mafanikio makubwa, kiasi kwamba uongozi wa klabu hiyo ukaamua kumuandalia sherehe la kumuaga ambapo hata hivyo alipatiwa fursa ya kucheza walau kwa dakika chache.

Mchezo wa mwisho uliopigwa majira ya saa 01:00 usiku uliwakutanisha Azam FC dhidi ya Simba SC, Azam wakiwa wenyeji wa mchezo huo katika dimba la Azam Complex Chamazi; mchezo huo ulimalizika kwa sare ya bao 1-1. Bao la Azam FC lilifungwa na Iddy Selemani Nado kunako dakika ya 43 kipindi cha kwanza huku bao la Simba likipachikwa kimiani  na mshumbuliaji mwenye nguvu na kasi Middie Kagere mnamo dakika za mwisho za mchezo huo.

Baada ya mchezo wa mwisho wa Azam FC na Simba makocha wa timu hizo waliweza kuzungumza na waandishi wa habari amabapo kocha msaadizi wa Azam FC Viver Bahati alisema kuwa timu yao ilicheza vizuri na malengo yao yalikuwa ni kupata alama tatu na kwamba mipango yao ilikuwa imekubali ndani ya dakika 45 za kwanza kabla Simba kusawazisha bao hilo. Aliongeza kuwa nafasi nyingi walizozikosa katika kipindi cha kwanza ndizo zilizoigharimu timu yao kushindwa kuibuka na ushindi hivyo kuruhusu goli katika dakika za mwisho za mchezo huo.

Kwa upande wa kocha wa Simba Gomez Da Rosa yeye alisema wazi kuwa kikosi chake kilifanya makosa mengi kipindi cha kwanza; kwamba hakukuwa na maelewano mazuri kati ya viongo na safu yake ya ulinzi jambo ambalo liliigharimu timu katika kipindi cha kwanza. Kocha huyo aliendelea kusema kuwa baada ya kugundua makosa hayo aliamua kufanya mabadiliko katika kipindi cha pili jambo ambalo lilipelekea kupata bao la kusawazisha kunako dakika za mwisho.

Kufuatia matokeo hayo ya mchezo wa mzunguuko namba 33 Ligi Kuu Bara, Simba, Young Africans, Azam FC na Biashara United zinabakia kwenye nafasi zao kama kawaida.  KMC inashikilia nafasi ya 5, Tanzania Prisons ya 6, Dodoma Jiji wao wanashikilia nafasi ya 7  wakati Namungo wenyewe wakishika nafasi ya 8. Polisi Tanzania anashikilia nafasi ya 9, Ruvu Shooting ya 10, Kagera Sugar nafasi ya 11 huku Mbeya City wao wakishikilia nafasi ya 12 katika msimamo wa ligi Kuu Bara.

Nafasi ya 13 inashikiliwa na Mtibwa Sugar huku Coastal Union ya Tanga wakijikongoja kwenda hadi nafasinya 14 ambapo kama akimaliza akiwa hapo basi atafanikiwa kwenda kucheza michezo ya mtoano (Play Off) ili kupata nafasi ya kushiriki tena Ligi Kuu kwenye msimu wa 2021/2022. Endapo timu hiyo ya Wagosi wa Kaya ikishindwa kupata matokeo dhidi ya Wanakurukumbi (Kagera Sugar) basi itakuwa imeaga ligi Kuu na kushuka kwenda kushiriki ligi daraja la kwanza.

Kwa hali hiyo, Coastal Union na Mtibwa Sugar zina kazi ya ziada ya kufanya katika michezo yao ya mwisho hali kadhalika JKT Tanzania amabaye kwa sasa ana alama 36 akishinda mchezo wa mwisho anaweza mtoa yeyote wa karibu yake.