Simba Bingwa Ngao ya Jamii

Timu ya Simba SC imefanikiwa kutwaa ubingwa wa Kombe la Ngao ya Jamii baada ya kupata ushindi kwenye mchezo wa fainali dhidi ya Young Africans uliopigwa Agosti 13, 2023 majira ya saa 1:00 usiku kwenye uwanja wa CCM Mkwakwani.

Mchezo huo uliomalizika kwa dakika 90 bila timu zote kufungana uliamuliwa kwa mikwaju ya penati Simba SC wakipata penati 3 -1 dhidi ya Young Africans.

Magoli ya Simba SC yamefungwa na Mzamiru Yassin, Willy Onana na Jean Baleke, wakati goli pekee la Young Africans limefungwa na Stephenie Azizi.

Kwa ushindi huo Simba inatawazwa ubingwa 2023/2024  mbele ya waliokuwa mabingwa (Young Africans) watetezi wa kombe hilo kwa misimu miwili mfululizo,  timu hiyo pia imekabidhiwa medali pamoja na tuzo zilizo kabidhiwa na viongozi mbalimbali akiwemo Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Wallece Karia.

Viongozi wengine walioambatana  na Rais ni Waziri wa Maendeleo ya jamii, jinsia, wazee na makundi maalum Mh. Dr Doroth Gwajima, Naibu Waziri Utamaduni, Sanaa na Michezo Mh. Hamis Mwinjuma, Mkurugenzi wa Uzuiaji Rushwa wa TAKUKURU Bi. Sabina Seja na Mwenyekiti wa Bodi ya Udhamini ya TFF Bwana Mohamed Abdulaziz.

Ikumbukwe hii ni mara ya tatu timu hizi kukutana kwenye fainali Ngao ya jamii, Mara mbili zote Young Africans walibeba kombe hilo kabla ya Simba kuvunja rekodi msimu huu na kubeba kombe hilo kwa mara ya kwanza mbele ya Young Africans.