Simba Mbeya City Zatoshana Nguvu Sokoine

Mchezo uliozikutanisha Mbeya City dhidi ya Simba SC  ulimalizika kwa timu hizo kutoshana nguvu baada ya kutoka sare kwa kufungana bao 1-1.

Mchezo huo uliopigwa Novemba 22, 2022 majira ya saa 10:00 jioni kwenye uwanja wa Sokoine jijini Mbeya ulikuwa na mvutano mkali huku Simba wakianza kwa kasi ya kusaka bao la mapema ambapo mnamo dakika ya 14 kipindi cha kwanza walikuwa tayariwamekwisha andika  bao; mfugaji akiwa Mzamiru Yassin (19) aliyemalizia pasi safi kutoka kwa Clatous Chota Chama.

Kipindi cha pili hali ya mchezo ilibadilika ambapo Mbeya City waliingia wakisaka bao la kusawazisha kwa udi na uvumba na kuifanya ngome ya ulinzi ya Simba kufanya makosa yaliyopelekea Mbeya City kupata bao la kusawazisha mnamo dakika ya 76 kupitia kwa Tariq Seif. Bao hilo liliufanya mchezo huo kumalizika kwa matokeo pacha.

Akizungumza baada ya mchezo huo Kaimu kocha Mkuu wa Simba Juma Mgunda alisema mechi ilikuwa ngumu kwa sababu kila timu ilikuwa imejipanga kupata matokeo chanya. Kocha Mgunda alieleza kuwa hayo ni mashindano na kwamba bado ni mapema kuzungumzia ubingwa lakini wao kama benchi la ufundi wamejipanga kwenda kurekebisha makosa waliyoyabaini kwenye mchezo huo ili waweze kufanya vyema kwenye michezo miwili inayofuata.

Kwa upande wa kucha msaidizi wa Mbeya City Anthony Mwamluma alisema anashukuru kwa wachezaji wao kwa kujituma na kusawazisha bao hilo. Aliongeza kuwa mechi hiyo ilikuwa ngumu na muhimu kwao hivyo si vibaya kwa wao kupata hata alama 1, kutokana na ubora wa timu waliyocheza nayo.

Mbali na matokeo hayo ya sare katika mchezo huo wa Mbeya City dhidi ya Simba wafungaji vinara wa timu hizo; Sixtus Sabilo na Moses Phiri walishindwa kuongeza idadi ya mabao kwenye hesabu yao hivyo kila mmoja kusalia na hesabu yake ya awali kama walivyoingia kwenye mchezo.

Katika mchezo mwingine wa mapema uliopigwa kwenye uwanja wa Liti  mjini Singida majira ya saa 08:00 ukiwakutanisha Singida Big Stars na KMC FC; timu ya Singida Big Stars ilifanikiwa kuiadhibu KMC bao 1-0. Bao hilo la Singida lilifungwa na Meddie Kagere (14) mnamo dakika ya 40 kipindi cha kwanza.

Kwa matokeo ya mechi hizo mbili Simba inafikisha alama 28 baada ya kucheza mechi 13, ikifikisha magoli 6 ya kufungwa sawa na Young Africans huku Mbeya City nao wakifikisha alama 19 baada ya kushuka dimbani mara 13. Kwa upande wa Singida Big Stars wao wanapqnda hadi nafasi ya 4 wakivuna alama 21 baada ya kushuka dimbani mara 12 wakati KMC wao wakisalia kwenye nafasi yao ya 12 baada ya kushuka dimbani mara 13.