Simba Queens Kukipiga na She Corporate Fainali
Timu ya Tanzania Simba Queens FC inatarajia kukipiga dhidi ya She Corporate timu kutoka Uganda kwenye hatua ya fainali michuano inayoendelea hapa nchini ya kufuzu Ligi ya Mabingwa wa Afrika kwa wanawake ukanda wa CECAFA.
Timu zote hizo zimefanikiwa kutinga kwenye hatua ya fainali baada ya kupata ushindi wa alama tatu kwenye mechi zao za nusu fainali, zilizo pigwa Agosti 24, 2022 uwanja wa Azam Complex.
Mchezo wa awali kwenye hatua hiyo ya nusu fainali ulimalizika kwa timu ya She Corporate kupata ushindi wa magoli 2-1 dhidi ya CBE FC ambapo iliwabidi She Corporate kujipanga upya baada ya kuruhusu bao la kusawazishwa lililofungwa na nahodha wa CBE Loza Abera Geinore dakika ya 62 baada ya wao kutangulia kupata goli kipindi cha kwanza mnamo dakika ya 20.
Hata hivyo bao la pili likiwekwa kambani dakika ya 72 na mchezaji Phiona Nabbumba na kufanya matokeo yasomeke She Corporate 2-1 CBE mpaka dakika 90 zinakamilika.
Simba Queens FC yenyewe ilishuka dimbani majira ya saa 1:00 usiku na kuiadabisha timu ya AS Kigali WFC kwa magoli 5-1, wafungaji wa magoli ya Simba Queens ni;Vivian Aquino Corazone aliyepachika magoli mawili, Opa Clement Tukumbuke, Aisha Juma Mnunka na Diana William Mnally akifunga hesabu ya jumla ya mabao 5.
Kocha Sebastian Nkoma alisema AS Kigali ni miongoni mwa timu bora kwenye michuano hiyo kwa mwaka huu, lakini licha ya ubora huo kwao haikuwapatia hofu kupambana kutafuta alama tatu kutokana na ubora wa kikosi chake.
Simba Queens haijapoteza mchezo wowote mpaka hatua hiyo, huku ikiwa na rekodi ya kuifunga She Corporate magoli 2-0 kwenye hatua ya makundi.
Fainali kati ya Simba Queens FC na She Corporate inatarajiwa kupigwa jumamosi ya tarehe 27, agosti mwaka huu. Mchezo mwingine utakao pigwa siku hiyo ni wakutafuta mshindi wa tatu kati ya CBE FC na timu ya AS Kigali ya nchini Rwanda.