Simba Queens Yaanza Ligi Kibabe

Pazia la Ligi Kuu ya Wanawake (SWPL) msimu 2021/2022 limefunguliwa Disemba 23, 2021 kwa kupigwa michezo miwili ambapo moja kati ya mechi zilizo chezwa ni kati ya Simba Queens (Mabingwa watetezi SWPL) iliyoanza kwa kishindo baada ya mchezo wao dhidi ya Ruvuma Queens kumalizika kwa Simba Queens kupata ushindi wa mabao 15-0.

Kipigo cha Ruvuma kilianza ndani ya dakika ya 10 wakianza kujifunga wenyewe kabla ya kujifunga bao lingine dakika ya 76,wafungaji wa mabao ya Simba Queens ni; Zena Khamis akiipatia timu yake mabao 3, Asha Djafar mabao 3, Opa Clement mabao 3 na bao moja lililofungwa na Aisha Juma kukamilisha jumla ya mabao 15.

Mechi ya Simba Queens na Ruvuma Queens ilichezwa kwenye uwanja wa Mo Simba Arena majira ya saa 10:oo jioni, huku mchezo mwingine ukipigwa kwenye uwanja wa Nyamagana Mwanza ambapo huko wenyeji Alliance Girls mchezo wao ulimalizika kwa wao kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Mlandizi Queens.

Ikiwa ndio mwanzo wa Ligi hiyo kwa msimu 21/22 Mkurugenzi wa Ufundi TFF Salum Madadi alisema kuwa matarajio ni kuwa na upinzani wa hali ya juu zaidi ya ilivyo kuwa msimu uliopita kwani kwa kipindi hiki anaamini walimu wametumia vizuri muda wao katika kuimarisha timu zao katika ushindani.

Aidha Salum Madadi alisisitiza kuhusu ahadi waliyoiweka TFF kwa viongozi wa vilabu kupitia kikao kilicho fanyika wiki hii kwamba watahakikisha ubora utaongezeka kwenye Ligi hiyo, sambamba na hayo aliwataka pia viongozi kila mmoja kwa nafasi yake aweze kutimiza majukumu yake inavyo takikana ili kukwepa makosa yasiyo ya lazima.

Michezo ya Ligi Kuu ya Wanawake (SWPL) itaendelea Disemba 24, 2021 kwa kupigwa michezo mingine minne, JKT Queens vs Oysterbay Girls, TSC Queens vs The Tigers Queens, Fountain Gate Princess vs Ilala Queens na Baobab Queens vs Yanga Princess mechi zote zikichezwa majira ya saa 10:00 jioni.