Simba Queens Yakabidhiwa Kombe TWPL

 

Mabingwa wapya Ligi Kuu ya Wanawake Tanzania (TWP) Simba Queens wamekabidhiwa kombe baada ya mchezo wao dhidi ya Geita Queens Juni 14, 2024 uliochezwa uwanja wa Azam Complex Chamazi.

Kwenye mchezo huo Simba Queens waliibuka na ushindi wa mabao 3-0, huku wakiwa na rekodi ya kuwa ndio pekee ambayo haijapoteza mchezo msimu huu 2023/2024, magoli ya Simba Queens yalifungwa na Aisha Juma, Elizabeth Wambui na Asha Rashid.

Akiiandikia goli la kutangulia timu yake mshambuliaji Aisha Juma ndani ya dakika ya 3 baada ya kupokea pasi ya Ritticia Nabbosa, huku Elizabeth Wambui akikomelea msumari wa pili dakika ya 34 kabla ya mchezaji mkongwe kwenye kikosi cha malkia hao wa K/Koo Asha Rashid kuweka kambani goli la tatu na la mwisho dakika ya 79.

Mabingwa hao wapya wamefanikiwa kubeba jumla ya alama 52 msimu huu baada ya kushinda mechi 17 na kupata sare kwenye mchezo mmoja dhidi ya Bunda Queens.

Mbali na ubingwa huo, mshambuliaji wa Simba Queens Aisha Mnuka amefanikiwa kufikisha idadi ya magoli 20 ambayo mpaka sasa yanamuhakikishia kubeba kiatu cha mfungaji bora wa msimu baada ya kuongoza kwa tofauti ya magoli mawili ukilinganisha na mchezaji wa JKT Queens Stumai Abdallah mwenye magoli 18.

Hata hivyo sherehe za ubingwa Kwa Mabingwa hao wa TWPL zilihudhuliwa na viongozi mbalimbali akiwemo mgeni rasmi Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania TFF Wallec Karia, alieambatana na Makamu wa pili wa Rais na Mwenyekiti wa Bodi ya ligi kuu Tanzania Steven Mnguto na Katibu Mkuu TFF Kidao Wilfred.

Sherehe hizo za Ubingwa pia zilinogeshwa na wadhamini kutoka The People’s Bank of Zanzibar Limited (PBZ) ambapo Kaimu Mkurugenzi wa benki hiyo Anwar Swaleh pamoja na wawakilishi wengine waliungana pamoja na viongozi wa TFF katika kufanikisha sherehe hizo.

Ikumbukwe matokeo ya michezo mingine iliyochezwa raundi ya mwisho kwenye viwanja mbalimbali yalikuwa; Yanga 1-0 Alliance Girls, Amani Queens 5-0Baobab Queens, JKT Queens 2-0 Ceasiaa Queens na Fountain Gate Princess 1-0 Bunda Queens.