Simba Queens yatamba mbele ya Yanga Princess

Ligi kuu ya wanawake imeendelea leo Aprili 25, 2023 Kwa mechi kadhaa kupigwa katika viwanja mbambali huku wababe Simba Queens wakibeba alama tatu katika dimba la Azam Complex, Chamazi baada ya kuifunga timu ya Yanga Princess goli 3-1.

Mchezo huo ulianza kwa timu zote mbili kucheza kwa kasi ya kawaida lakini baadae Simba Queens ilionekana kuutawala mchezo kwa kipindi chote cha Kwanza hata hivyo juhudi hizo hazikuzaa matunda na milango ya timu zote mbili kuendelea kuwa migumu hadi kipindi cha Kwanza kinamalizika.

Magoli ya Simba Queens yalifungwa katika kipindi cha pili cha mchezo, Aisha Mnuka akifunga magoli 2 dakika ya 60 na katika dakika za nyongeza za kipindi cha pili huku Jentrix Shikangwa akifunga goli moja . Goli la kufutia machozi kwa Yanga Princess lilifungwa na Kaeda Wilson na hivyo mchezo kumalizia kwa Simba Queens kupata ushindi wa goli 3 -1

Kocha Mkuu wa Simba Queens Juma Mgunda alisema ” Tunamshukuru Mungu mchezo umemalizika salama na tumepata alama tatu muhimu, ulikua mchezo mzuri na wa ushindani tunashukuru umepita tunasubiri mchezo ujao”.

Naye Kocha mkuu wa Yanga Princess Charles Halubono aliwapongeza wachezaji wake kwa mchezo wa Leo licha ya kupoteza huku akikiri kwamba kikosi cha Simba Queens kilikua Bora na walitumia makosa waliyoyafanya kuwaadhibu. Dabi imeisha tunakwenda kujipanga kwa mchezo unaofuata dhidi ya Fountain Gate princess.

Kwa matokeo hayo Simba Queens anaendelea kusalia kileleni kwa alama 34 wakati Yanga Princess akiendelea kushikilia nafasi ile Ile ya nne akiwa na alama 21

Mchezo mwingine wa Ligi kuu ya wanawake uliochezwa Leo ulikua Kati ya JKT Queens dhidi ya Amani Queens na mchezo huo ulimalizika Kwa timu ya JKT Queens kuibuka na ushindi wa goli 4-0. Magoli ya JKT Queens yalifungwa na Stumai Abdallah, Fatuma Makusanya, Jamila Rajabu huku mchezaji wa Amani Queens Fumukazi Ally akijifunga goli moja.