Simba Queens Yazidi Kujibebea Pointi SWPL

Ni katika muendelezo wa mechi za Ligi Kuu ya Wanawake (SWPL) ambayo ipo kwenye mzunguko wa tatu, mchezo nambari 14 uliowakutanisha Ilala Queens na Simba Queens umemalizika kwa mabingwa watetezi wa Ligi hiyo Simba queens wakiendelea kujibebea alama tatu kwa ushindi wa mabao 4-1.

Mchezo huo ulichezwa kwenye uwanja wa Karume jijini Dar es Salaam Januari 03, 2022 majira ya saa 10:00 jioni ambapo mchezaji Opa Clement aliweza kuifungia timu yake mabao matatu, huku bao moja wapo akilifunga kwa mkwaju wa penalti na lile la kwanza akipokea assist nzuri kutoka kwa Koku Kipanga. Mchezaji ambaye pia ni mfungaji wa bao la tatu kwa Simba Queens.

Mabao manne kwa Simba Queens na goli moja la pekee kwa Ilala Queens lililofungwa na mchezaji Fatuma Hassan katika kipindi cha pili cha mchezo.

Kocha mkuu wa Simba Queens Sebastian Nkoma lisema kuwa, mechi haikuwa rahisi kwa upande wao licha ya mashambilizi ya nguvu waliyo fanya wachezaji wake. Sambamba na hayo pia kocha amewataka mashabiki wa klabu hiyo kuendelea kuwa na Imani na mwenendo wa timu yao kwani lengo lao hasa ni kuendelea kutetea nafasi ya ubingwa katika msimu huu 21/22.

Kwingineko kocha mkuu wa Ilala Queens Twaha Beimbaya yeye alikipongeza kikosi chake kwa mchezo mzuri, aidha kwa upande mwingine aliwaahidi mashabiki kupata burudani ya mpira mzuri kutoka kwenye timu hiyo kwani anaamini licha ya ugeni wao kwenye ligi bado wanaendelea kuimarika na kuwa bora zaidi.

Matokeo ya mechi nyingine za raundi ya tatu; Mlandizi Queens 1-2 Baobab Queens, The Tiger Queens 2-3 Fountain Gate Princess, Ruvuma Queens 0-3 Alliance Girls, Oysterbay Girls 2-0 TSC Queens na mechi nyingine iliyochezwa Januari 2, 2022 Yanga Princess alipata ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya JKT Queens.

Kwa matokeo hayo Simba Queens anaendelea kusalia kileleni kwa jumla ya alama 9 akimshusha Yanga Princess mpaka katika nafasi ya 3 akiwa na alama 7, wakitofautiana kwa idadi ya magoli na Fountain Gate Princess akishikilia nafasi ya pili na mwishoni akiendelea kung’ang’ana Ruvuma Queens aliyefungwa magoli 20 mpaka katika mzunguko huo. Wakati Alliance Girls ndiyo timu pekee ambayo haijaruhusu bao lolote la kufungwa katika mechi zake zote.