Simba SC Kukutana na Young Africans Fainali Ngao ya Jamii

Mchezo wa pili nusu fainali Ngao ya jamii umemalizika kwa timu ya Simba SC kupata ushindi wa magoli 4-2 yaliyopatikana kwa changamoto ya mikwaju ya penati dhidi ya timu ya Singida Fountain Gate.

Magoli ya penati kwa Simba SC yalifungwa na wachezaji Luis Miquesson, Saido Ntibazonkiza, Mzamiru Yassin na goli la mwisho likiwekwa kambani na Moses Phiri alieingia kipindi cha pili kutokea benchi.

Akizungumza baada ya mchezo kocha mkuu wa Simba SC Loberto Oliveira alikipongeza kikosi chake kwa kufanikisha lengo la kufuzu hatua ya fainali, huku akiwasifu wapinzani wake kwa mchezo mzuri.

Oliveira alimpongeza pia golikipa wake Ally Salim kuwa sehemu ya mchango wa kuifanikisha timu yao kufika fainali.

Kwa matokeo hayo Simba SC itacheza fainali dhidi ya Young Africans Agosti 13,2023 majira ya saa 1:00 usiku kwenye uwanja wa CCM Mkwakwani baada ya kumalizika kwa mchezo wa kumtafuta mshindi wa tatu kati ya Azam FC na Singida Fountain Gate utaopigwa majira ya saa 9:00 alasiri.