Simba Yabanwa Mbavu na Ruvu Shooting Kwenye Uwanja wa Mkapa Dar es Salaam
Mchezo kati ya Simba na Ruvu Shooting umechezwa hii leo kwa timu hizo kutoshana nguvu baada ya kutoka sare ya bao 1-1.
Mchezo huo uliopigwa katika dimba la Mkapa majira ya saa 10:00 jion ulizikutanisha timu hizo mara baada ya kukaa nje ya uwanja kwa takribani miezi mitatu kutokana na kuibuka kwa ugonjwa wa Covid 19 unaosababishwa na virusi vya Corona.
Ni Simba ndio waliokuwa wakwanza kupata goli mnamo dakika ya 12 kupitia kwa mchezaji jezi namba 23 Shiza Kichuya baada ya kuukuta mpira ukizengea zengea kwenye eneo la goli mara baada ya goli kipa wa Ruvu Shooting kupangua kombora kali, ndipo mchezaji huyo jezi 23 na aliyerejea hivi karibuni katika kikosi cha wekundu wa hao kupiga shuti kali lililomshinda mlinda mlango na kutinga nyavuni.
Ruvu Shooting walijipanga upya na kuanza kupeleka mashambulizi huku wakiwa na tahadharsi kubwa na mnamo dakika za lala salama za kipindi cha kwanza maafande hao walifanikiwa kusawazisha goli lililofungwa na Fully Manganga akiunganisha kwa kichwa mpira wa kona. Goli hilo lilizifanya timu hizo kuelekea katika mapumziko zikitoshana nguvu.
Kipindi cha pili kilianza kwa mashambulizi ya kushitukiza kwa kila upande huku kosa kosa zikiwa nyingi kwa pande zote. Lakini ni Ruvu Shooting ndio walioonesha kulisakama sana lango la Simba ambapo wajeda hao waliweza kutengeneza nafasi nyingi na za hatari zaidi kabla ya Simba kuzinduka katika dakika za majeruhi na wao kupeleka mashambulizi katika lango la wapinzani wao. Hata hivyo, juhudi hizo hazikuweza kuzaa matunda na kufanya mchezo huo kumalizika kwa sare ya goli 1-1.
Kocha wa Ruvu Shooting Salum Mayanga amewapongeza wachezaji wake na kusema wameonesha kiwango kizuri licha ya kushindwa kuzitumia nafasi nyingi za wazi ambao huenda zingewawezesha kuibuka na ushindi. Juhudu za kumpata Kocha wa Simba Sven Vandenbroeck hazikuzaa matunda kutokana na zuio la kuhojiana ana kwa ana na makocha mara baada ya mchezo.
Kikosi cha Simba kilichoanza ni Aishi Manula, Shomar Kapombe, Gadiel Michael, Erasto Nyoni, Pascal Wawa, Mzamiru Yassini, Hassani Dilunga, Luis Miquisson, Meddie Kagere, John Bocco, na Chiza Kichuya, huku wale wa akiba wakiwa; Ally Salim, Mohammed Hussein, Yusuph Mlipili, Said Hamis, Deogratias Kanda, Miraji Athumani na Francis Kahata.
Kwa upande wa Ruvu Shooting ni; Mohamed Makaka, Omary Kindamba, Kassim Simbaulanga, Rajab, Zahir, Baraka Mtuwi, Zuberi Dabi, Abdallahman Mussa, Shabani Msala, Graham Naftal, Fully Manganga na William Patrick; huku wale wa akiba wakiwa ni Abdallah Rashid, Mau Bofu, Renatus Kisase, Moses Shaban, Said Dilunga, Sadat Mohamed pamoja na Jamal Mnyate. Kwa mchezo huo Simba SC anaendelea kubaki kileleni(72) akifuatiwa kwa karibu na Azam FC na Mabingwa wa Kihistoria Yanga SC wenye alama 54.