Simba yalazimwishwa sare kwa Mkapa

Mchezo uliopigwa katika Dimba la Mkapa majira ya saa moja usiku umemalizika kwa timu hizo kutoshana nguvu baada ya mtanange huo kutamatika kwa sare ya kufungana bao 1-1.

Mchezo huo ulioanza taratibu huku timu zote zikishambulia kwa kuviziana kwa kuhofia kupoteza mchezo. Lakini baada ya muda wa dakika 28 kufika Simba wakafanikiwa kupata penati ambayo ilikwenda kupigwa na Chriss Mugalu ambaye alishindwa kuupachika mpira huo kimyani na kuufanya mchezo huo kwenda suluhu mpaka dakika 45 za kipindi cha kwanza.

Kunako dakika ya 30 mchezaji wa Tanzania Prisons Jamanne Elifadhil (04) alipata kadi nyekundu baada ya kucheza mpira usio wa kiungwana kwa mchezaji wa Simba na hivyo kuifanya timu yake kwenda katika mapunziko ikiwa na wachezaji pungufu jambo ambalo liliipatia faida Simba na kuongeza mashambulizi zaidi.

Kipindi cha pili kilianza na kasi, Simba wakitaka kupata bao ili kujihakikishia ushindi bado Tanzania Prisons walionekana kuwa wagumu na hawakutaka kuachia nafasi kirahisi na hivyo kuwapa wakati mgumu Simba jinsi ya kupata bao la kuongoza.

Kunako dakika ya 10 ya kipindi cha pili Tanzania Prisons walifanikiwa kuandika bao la kuongoza kwa mpira wa faulo uliopigwa na Salumu Mashaka Kimenya(14) ambaye alipiga mpira huo kiufundi na kumpoteza mlinda mlango wa Simba  Aishi Salum Manula bao lilidumu kwa dakika takribani 33 kabla Simba hawajasawazisha bao hilo kupitia kwa Luis Micquissone, bao hilo liliwaacha hoi Wajelajela hao ambao walikwisha kujihakikishia kuondoka na alama tatu kwa mara nyingine baada ya mchezo wa kwanza kufanya hivyo wakiwa kwao Nelson Mandela.

Mchezaji aliyeonekana nyota wa mchezo huo alikuwa ni Mlinda mlango wa Tanzania Prisons Jeremia Kisubi ambaye aliokoa michomo mingi ikiwa ni pamoja na penati iliyopigwa na Chriss Mugalu.

Baada ya mchezo huo kocha wa Simba Gomes Da Rosa alisema kuwa mchezo huo ulikuwa mgumu na kwamba hakufurahishwa na matokeo hayo. Aliongoza kuwa mchezo huo ulimpa wakati mgumu namna gani ya kushinda kutokana na mfumo walioingia nao wapinzani wake Tanzania Prisons. Licha ya kusema bado aliwapongeza wachezaji wake kwa kujituma na kupambana mpaka dakika ya mwisho bila kukata tamaa na kufanikiwa kurejesha bao hilo katika dakika za mwisho za mchezo. Kocha huyo alielezea tukio la Chriss Mugalu kukosa penati kuwa ni jambo la kawaida na kwamba hawezi mlaumu kwa kosa hilo.

Kwa upande wa kocha  msaidizi wa Tanzania Prisons Ibrahimu Kazumba alisema kuwa timu yake imecheza vizuri kwani walipata kadi nyekundu katika kipindi cha kwanza na hivyo kuwalazimu kucheza kwa kujilinda kutokana na ubora wa timu ya Simba. Kocha huyo aliwasifia wachezaji wake kwa kuhemu na kufuata maelekezo yake ambayo ndio yaliwasaidia kupata alama moja. Hata hivyo kocha huyo hakusita kukisifia kikosi cha Simba kwa ubora kilionao katika maeneo yote.

Kwa matokeo hayo yanaifanya Tanzania Prisons kuongeza alama moja na kufikisha jumla ya alama  28 baada ya kucheza mechi 22  wakati Simba wao wakifikisha alama 46 wakicheza mechi 20, hivyo kubakiza alama 4 pekee kuwafikia vinara wa ligi hiyo Young Africans ambao wao wanaalama 50 baada ya kushuka dimbani mara 23.