SIMBA SC Vs YANGA SC

Simba yatinga Fainali FA, Kukutana Uso kwa Uso na Namungo FC

Hatimaye mbwembwe, kejeli na vijembe vya watani wa jadi ‘Simba na Yanga’ zimemalizika baada ya Yanga kukubali kichapo cha bao 4-1 katika mchezo uliochezwa 12 Julai, 2020 kwenye uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Mchezo huo uliopigwa majira ya saa 11:00 jioni ulikuwa mkali ambapo katika dakika chache za kipindi cha kwanza Yanga walionekana kuanza kwa kasi, lakini baada ya dakika 15 walionekana kupwaya na Simba kuanza kuutawala mpira.

Mnamo dakika ya 21 tu ya mchezo, Simba walifanikiwa kuandika bao la kwanza; bao lililofungwa na Gerson Fraga jezi namba 04  aliyemalizia mpira uliokuwa ukizagaazagaa katika eneo la 18. Mpaka timu hizo zinakwenda mapumziko Simba ilikuwa mbele kwa bao 1-0.

Kipindi cha pili kilianza huku Simba wakionesha nia thabiti ya kutaka kucheza Fainali hizo za FA, na baada ya dakika chache tu wakafanikiwa kuongeza bao la pili kupitia kwa mchezaji jezi namba 17 Clatous Chama. Hazikupita dakika nyingi Luis Miquissone akakomelea msumari wa tatu.  Hata hivyo Yanga hawakukata tamaa wakafanya mashambulizi na kufanikiwa kupata bao kupitia kwa mchezaji jezi namba 06 Feisal Salum (Feitoto). Mnamo dakika za lala kwa buriani Mzamiru Yassin akaongeza msumari wa moto na kuwafanya mashabiki wa Yanga kuondoka uwanjani kabla ya mpira kwisha. Mpaka  dakika 90 zinakamilika Simba 4-1.

Kocha wa Yanga Luc Eymael alisema kuwa kikosi chake kimezidiwa kimchezo na kwamba wachezaji wake walikosa umakini wa kuzitumia nafasi chache walizozipata. Kwa upande wa kocha wa Simba Sven Vandernbroeck alisema kuwa kikosi chake kilicheza vizuri katika mchezo huo na kwamba kufuatia matokeo hayo kocha huyo alitoa siku mbili  za mapumziko kwa kikosi chake.

Vikosi vilivyoingia uwanjani kwa upande wa Simba ni; Aishi Manula, Shomar Kapombe, Mohammed Hussein, Kennedy Juma, Pascal Wawa, Jonas Mkude, Luis Miquissone, Gerson Fraga, John Bocco, Clatous Chama na Francis Kahata. Wachezaji wa akiba walikuwa ni Beno Kakolanya, Gadiel Michael, Erasto Nyoni, Mzamiru Yassin, Hassan Dilunga, Meddie Kagere na Miraji Athuman.

Kwa upande wa Yanga kikosi cha kwanza kilikuwa na; Metacha Mnata, Juma Abdul, Jafar Mohamed, Lamine Moro, Said Makapu, Papy Tshishimbi, Feisal Salum, Haruna Niyonzima, Deus Kaseke, David Molinga na Benard Morrison. Wale wa akiba walikuwa ni; Farouk Shikalo, Kelvin Yondani, Adeyun Saleh, Abdul Aziz Makame, Patrick Sibomana, Mrisho Ngassa (Anko) na  Ditram Nchimbi.

Kwa matokeo hayo ya mchezo huo wa watani wa jadi, Simba itakwenda kucheza fainali dhidi ya Namungo FC ambayo iliifyatua Sahare All Stars kwa goli 1-0 katika mchezo uliochezwa tarehe 11 Julai 2020 huko Mkwakwani Jijini Tanga. Fainali hizo za Kombe la FA zitachezwa Agosti Mkoani Rukwa.