Want create site? Find Free WordPress Themes and plugins.

Simba SC Yaendelea Kuweka Heshima Kwa Mkapa

Timu ya Simba SC imefanikiwa kulinda heshima yake baada ya kuifumua Mbeya City kwa jumla ya mabao 3-0 katika mchezo uliopigwa Juni 16, 2022 kwenye uwanja wa Benjamin Mkapa majira ya saa 1:00 usiku.

Simba walikuwa wa moto katika mchezo huo baada ya kuutawala mpira kwenye vipindi vyote licha ya Mbeya City kuingia na mbinu ya kuzuia bado haikuweza kuwasaidia kwani mbinu yao hiyo ilidumu kwa dakika 36 pekee za kipindi cha kwanza cha mchezo huo.

Simba walifanikiwa kuandika bao la kwanza mnamo dakika ya 37 ya mchezo, bao hilo likifungwa na mchezaji jezi namba 10 Pape Othuman Sakho kwa mkwa wa penati baada ya mlinda mlango wa Mbeya City kumchezea madhambi ndani ya eneo la 18. Hadi timu hizo zinakwenda mapumziko ubao wa matokeo ulisomeka 1-0.

Kipindi cha pili Simba walifanikiwa kuandika mabao mawili ambapo Sakho alirejea tena kambani na baadaye Peter Banda (11) naye akashindilia msumari wa moto kunako dakika za mwishoni. Ushindi huo unaiwezesha Simba kufikisha alama 54 ikiwa nyumaa kwa alama 13 dhidi ya watani wao Young Africans.

Katika mchezo mwingine uliopigwa mapema majira ya saa 10:00 jioni Ilulu Lindi, uliwakutanisha Namungo dhidi ya Polisi Tanzania na matokeo yalikuwa ni 2-1 ambapo Polisi Tanzania walifanikiwa kuibuka na ushindi dhidi ya wenyeji Namungo FC.

Matokeo ya mchezo huo yaIliwezesha Polisi Tanzania kupanda hadi nafasi ya 6 ikifikisha alama 36 baada ya kushuka dimbani mara 27 wakati Namungo wao wakisalia kwenye nafasi ya 5 nao baada ya kushuka dimbani mara 27 pia.

Ligi Kuu ya NBC inaelekea ukingoni kwani bingwa amekwisha kutawazwa. Hata hivyo, timu zote bado zimeonekana kujipanga kuhakikisha zinapata matokeo katika kila mchezo kwani kuna mgawanyiko wa makundi ambapo baadhi ya timu zimeisha jihakikishia kushiriki ligi ya mabingwa ambazo ni Young Africans na Simba SC.

Kundi la pili, linaundwa na timu zile zinazowania kumaliza katika nne bora ili ziweze kupata nafasi ya kushiriki michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika; timu hizo ni Azam FC, Geita Gold, Namungo, Polisi Tanzania, Kagera Sugar na Coastal Union. Kundi jingine ni lile lisilo na cha kupoteza huku kundi la mwisho ni la timu ambazo ziko katika hatari ya kushuka daraja, kundi hili linaundwa na timu kama vile; Mbeya Kwanza, Biashara United, Tanzania Prisons, Ruvu Shooting, Dodoma Jiji na Mtibwa Sukari.

 

 

Did you find apk for android? You can find new Free Android Games and apps.