Simba Yamaliza Duru ya Kwanza Kibabe Ugenini
Timu ya Simba SC imefanikiwa kumaliza mchezo wake wa 15 katika duru ya kwanza kwa kuvuna ushindi mnono baada ya kuifumua Coastal Union jumla ya mabao 3-0 Wagosi hao wakiwa kwenye uwanja wao wa nyumbani Mkwakwani Tanga.
Katika mchezo huo uliopigwa Disemba 3, 2022 kwenye majira ya saa 10:00 kulikuwa na ushindani mkubwa hasa katika kipindi cha awali ambapo wenyeji Coastal Union walionekana kuwa wabishi kuchaniwa nyavu zao kwa muda wote wa dakika 45 za kwanza.
Hali ilibadilika mara baada ya timu hizo kurejea katika kipindi cha pili ambapo zilipita yapata dakika 12 kwa timu ya Simba kuwa imeandika bao la kuongoza, bao hilo likifungwa na Moses Phiri baada ya kupokea pasi maridadi kutoka kwa kiungo fundi raia wa Zambia, Clatous Chota Chama aliyepiga pasi mpenyezo iliyomkuta Phiri naye hakufanya makosa akapachika kambani.
Kunako dakika ya 64 Moses Phiri aliwarejesha kati, kwa mara ya pili baada ya kufunga goli kwa penati iliyotokea baada ya mlinzi wa Wagosi wa Kaya kumfanyia madhambi beki kiraka wa Simba, Shomari Kapombe ambapo mwamuzi aliamuru mkwaju wa penati. Kunako dakika za lala kwa buriani (90+) Mwamba wa Lusaka Chama akakomelea msumari wa tatu uliowafanya Wagosi wa Kaya kukata tamaa ya kutafuta walau bao la kufutia machozi.
Akizungumza baada ya mchezo huo kocha wa Coastal Union Yusuph Chipo alisema timu yake ilizidiwa hasa katika nusu ya pili, kwani katika kipindi cha kwanza walifanikiwa kuwadhibiti Simba kikamilifu. Aliongeza kuwa mchezo wa mpira wa miguu ni wa makosa, mmoja anapofanya makosa ndipo mwingine anapata nafasi ya kushinda hivyo wachezaji wake walijisahau wapinzani wakawadhibu.
Kwa upande wake Juma Mgunda, kaimu kocha Mkuu wa Simba alisema alipomaliza kipindi cha kwanza akawa kawasoma vijana wa Coastal Union hivyo muda wa mapunziko alienda kuwaelekeza wachezaji wake nini cha kufanya ili kuweza kupata matokeo kwenye mchezo huo. Jambo amablo anashukuru wachezaji wake walilifanya kwa umakini mkubwa hatimaye kufanikisha adhima yao ya kukamilisha duru ya kwanza kwa kukusanya alama 6 kwenye mechi mbili.
Katika mchezo wa mapema uliopigwa majira ya saa 8:00 mchana ukiwakutanisha Dodoma Jiji na Ruvu Shooting; timu ya Dodoma Jiji ilifanikiwa kuibuka na ushindi wa bao 2-1 kwenye mchezo uliochezwa katika dimba la Liti Mjini Singida. Wafungaji wa magoli kwenye mchezo huo walikuwa; Salum Kipaga dakika (04), Hassan Mwaterema (24) na Ally Mwale dakika ya (75).
Matokeo hayo yanaifanya Dodoma Jiji kufikisha alama 15 huku Coastal Union wao wakibakia na na alama zao 12 wakati Simba wenyewe wakipasua mawimbi na kufikisha alama 34.