Simba, Young Africans Bado Zinanafasi Kutinga Nusu Fainali CAFCL
Wawakilishi wa Tanzania kwenye Michuano ya Klabu Bingwa Afrika Simba SC na Young Africans SC, bado wananafasi ya kusonga mbele kwenye michuano hiyo mikubwa Barani Afrika kwa ngazi ya vilabu licha ya kutopata ushindi katika michezo yao ya awali iliyochezewa nyumbani kwa Mkapa tarehe29 na 30 Machi, 2024.
SimbaSC ndiyo ilianza kushuka dimbani Machi 29 majira ya saa 3:00 usiku mchezo huo ikiwa na ushindani mkali licha ya wenyeji hao kuruhusu bao, bado waliweza kuonesha kandanda safi ambapo walifanikiwa kumiliki mpira kwa kiwango kikubwa huku wapinzani wao Al-Ahly wakitumia kosa moja lililofanywa na walinzi wa Simba SC kupata bao la kuongoza mnamo dakika ya 5, likifungwa na Ahmed Kouka na kudumu kwa dakika zote za mchezo huo.
Kwa upande wa watani wao wa jadi, Young Africans SC wenyewe walishuka dimbani Machi 30, 2024 kuvaana na mabingwa wa michuano mipya ya African Football League (2023) Mamelodi Sundowns kutoka Afrika Kusini mchezo ambao ulimalizika kwa timu hizo kutoka suluhu tasa.
Aidha, katika mechi hiyo ya Young Africans dhidi ya Mamelodi Sundowns; timu ya Mamelod ndiyo ilitawala zaidi dimba kwa kuwa na umiliki mkubwa wa mpira huku wenyeji Young Africans wakionekana kuiziba mianya yote ambayo ingeweza kuwaletea madhara katika vipindi vyote. Hatimaye kufanikiwa kutoruhusu bao lolote jambo ambalo kwao bado linawapa nafasi zaidi.
Baada ya mchezo huo kwisha kocha Miguel Gamond wa Young Africans alisema kikosi chake kimecheza vizuri kimbinu, licha ya kuzidiwa umiliki wa mpira bado hakikuruhusu bao lolote wala kuacha mianya ya kushambuliwa zaidi, baadala yake kilicheza kwa kuwaheshimu wapinzani huku lengo likiwa ni kuimaliza mechi pasipo kuruhusu bao ili kujipanga vyema kwa ajili mchezo wa pili.
Kocha Rulani Mokwena wa Mamelodi Sundowns naye alisema kuwa mbinu waliyoingia nayo Young Africans kwenye mchezo huo iliwapa shida kutengeneza nafasi ya kuandika mabao kwani wachezaji wake ilibidi watumie muda mwingi kucheza katika eneo lao kuliko kushambulia ikiwa ni mbinu ya kutaka kuwavuta wapinzani wao wasogee.
Hata hivyo, kocha huyo alisema kuwa hatua hiyo ya robo fainali inaamuliwa na dakika180; na kwamba dakika 90 za kwanza zimekwisha hivyo akili zote zinaelekezwa kwenye mchezo wa mwisho utakaopigwa Afrika Kusini.
Nchini Afrika Kusini timu ya Young Africans itahitaji sare yeyote ya kufungana ili isonge mbele huku Mamelodi Sundowns wenyewe wakitakiwa kupata ushindi wowote. Kwa upande wa Simba SC wao watahitaji kwenda kushambulia zaidi ili wapate bao la kusawazisha kabla ya kuandika bao la pili na la ushindi; lakini endapo matokeo ya jumla yakiwa pacha ndani ya dakika 180 itawalazimu kwenda hadi dakika 120, ama kuingia katika hatua ya changamoto ya mikwaju ya penati kwani hatua hii lazima mmoja atoke.