Simba Young Africans Watunishiana Misuli kwa Mkapa

Mchezo wa Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara, uliowakutanisha watani wa jadi Simba SC na Young Africans kwenye dimba la Benjamin William Mkapa majira ya saa 11:00 jioni umemalizika kwa timu hizo kutoshana nguvu kwa kutoka suluhu tasa.

Mchezo huo uliopigwa Disemba 11, 2021 ulioonekana kuwa ni kati ya mechi bora msimu wa 2021/2022 ulianza taratibu huku kila timu ikionesha ufundi wa hali ya juu licha ya kutofungana bao lolote. Timu ya Simba ilifanikiwa kutengeneza nafasi  nyingi za mashambulizi kuelekea kwa wapinzani wao, hali iliyopelekea Young Africans kurudi nyuma kuzuia kwa kipindi kirefu.

Kipindi cha pili hakikuwa kigumu kwa timu zote mbili mara baada ya vikosi kuwa vimesomana vizuri; hivyo wote walikuwa wakishambuliana kwa zamu huku makocha wote wakifanya mabadiliko ya hapa na pale kila mmoja akiwa na lengo la kuongeza ulinzi na mashambulizi pia ili kutafuta bao lolote sambamba na kuzuia bao lisifungwe. Hali iliendelea hivyo hadi dakika 90 za mchezo huo zinakamilika; timu zote zikitoka na alama moja.

Baada ya mchezo kumalizika kocha mkuu wa klabu ya soka ya Simba Pablo Franco alisema kuwa amefurahishwa na mchezo mzuri wenye viwango kwa timu zote mbili, huku akikipongeza kikosi chake kwa kucheza vizuri dakika zote 90 za mtanange huo hasa katika kipindi cha pili ambapo wapinzani wao walionekana kurudi wakiwa bora zaidi.

Kwa upande wa kocha wa Young Africans Nasreddine  Nabi, yeye alisema kuwa mechi ilikuwa ya ufundi ambapo timu zote zilishambuliana kwa awamu huku zikionesha viwango vilivyo shabihiana takribani kwa kila kitu.

Kikosi kilichoanza kwa Simba Sc; Aishi Manula(JN 28), Shomari Kapombe(JN 12), Mohamed Hussein(JN 15), Joash Onyango(JN 16), Henock Inonga(JN 29), Jonas Mkude(JN 20), Hassan Dilunga(JN 24), Sadio Kanoute(JN 13), Medie Kagere( JN 14), Kibu Denis(JN38) na Bernard Morrison(JN 03).

Kikosi kilichoanza Young Africans; Djigui Diarra(JN 39), Djuma Shaban(JN 21), Kibwana Shomari(JN 15), Bakari Mwamnyeto(JN 03), Dickson Job(JN 05), Khalid Aucho(JN 08), Jesus Moloko(JN 12), Yannick Bangala(JN 04), Fiston Mayele(JN 09), Feisal Salum(JN 06) na Saidi Ntibazonkiza(JN 60).

Kwa matokeo hayo yanaibakisha Young Africans akiwa na alama 20 akifuatiwa na Simba SC mwenye alama 18 wakati Mbeya City wao wakiendelea kusalia katika nafasi ya tatu wakiwa na alama 14  huku Mbeya Kwanza naye akiwa katika nafasi ya tatu kutoka mwisho na aliyekamatia mkia akibaki kuwa Mtibwa Sugar aliye na alama 2 pekee katika saba alizocheza.

Ligi Kuu Soka Bara itaendelea kutimua vumbi Disemba 12, 2021 kwa michezo miwili kupigwa ambapo katika uwanja wa Manungu Complex utapigwa mchezo kati ya Mtibwa Sugar na Biashara United majira ya saa 10:00 jioni, wakati mchezo mwingine utawakutanisha Azam FC dhidi ya Kagera Sugar kwenye uwanja wa Azam Complex Chamazi majira ya saa 1:00 usiku.