Singida Big Stars Yaweka Rekodi Mpya Dhidi ya Namungo

Mchezo kati ya timu ya Singida Big Stars na Namungo FC uliopigwa Disemba 2, 2022 kwenye uwanja wa Liti mjini Singida ulimalizika kwa SBS kuandika rekodi mpya ya ushindi wa zaidi ya mabao mawili baada ya kufanikiwa kufunga jummla ya mabao 3-0.

Ushindi huo ni wa kwanza kwa SBS tangu ipande Ligi Kuu ya NBC ambapo kumbukumbu zinaonesha kuwa ushindi mkubwa iliyowahi kuupata timu hiyo ni ule wa bao 2-1 iliyoupata katika uwanja wake wa nyumbani. Awali timu hiyo yenye makao makuu yake mjini Singida ilikuwa ikipata ushindi wa bao moja moja, tofauti na mchezo huo dhidi ya Namungo FC.

Mabao ya Singida Big Stars yalipachikwa na; Said Ndemla dakika ya (27), Meddie Kagere (66) na Amis Tambwe (90+). Ushindi huo wa bao 3-0 unaifanya timu hiyo kuendelea kushikilia nafasi ya nne ikiwa na alama 27 baada ya kucheza michezo 14 huku ikisubiri mchezo wa kukamilisha duru ya kwanza kwa matumaini makubwa.

Kocha wa SBS Hans van der Pluijm alisema amefurahishwa na matokeo hayo na kwamba anawapongeza wachezaji wake kwa jitahada zao. Aidha, kocha Pluijm alidai kuwa ligi bado ni ngumu na kwamba wao wanampango mahsusi wa kuhakikisha wanakusanya alama zaidi katika kila mchezo ili kujihakikishia kushika nafasi ya juu kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya NBC.

Wakati Pluijm akieleza hayo, kwa upande wa kocha msaidizi wa kikosi cha Namungo (The Southern Killers) Shedrack Nsajigwa yeye alieleza kuwa wachezaji wake walijitahidi kutafuta matokeo lakini hali haikuwaendea vyema kama walivyotaraji. Nsajigwa aliwapongeza wapinzani wao akisema kuwa walicheza vizuri na kuwazidi hatimaye kuweza kupata matokeo. Hata hivyo, kocha huyo alisema bado ligi inaendelea na kwamba makosa yaliyojitokeza watayafanyia kazi haraka iwezekanavyo ili kujiweka sawa kwa ajili ya michezo mingine.

Katika mchezo wa pili uliokuwa ukipigwa kwenye dimba la Kaitaba Bukoba, timu ya Kagera Sugar nayo ilifanikiwa kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhdi ya Ihefu FC kutoka Mbalali Mbeya. Wapachikaji wa mabao ya Kagera Sugar walokuwa ni; Erick Mwijage dakika (67) na Hamis Kiiza (83). Mchezo huo ulipigwa majira ya saa 10:00 jioni sambamba na ule wa SBS dhidi ya Namungo FC.

Matokeo ya mchezo huo kati ya Wanankurukumbi na Ihefu FC, yanaifanya Kagera Sugar ifikishe alama 21 huku ikitoka nafasi ya 9 na kukwea hadi nafasi ya 6 ikizishusha Mtibwa Sugar na Mbeya City kwa tofauti ya magoli ya kufunga na kufungwa wakati huo huo ikiiacha Namungo FC yenye alama (20) kwa tofauti ya alama moja pekee.