Soka la Ufukweni Raundi ya 11 Kuendelea Fukwe za Coco Beach

Ligi kuu ya Soka la ufukweni almaarufu kama Beach Soccar inaendelea kuchanja mbuga ambapo mechi sita zinatarajiwa kupigwa kwenye fukwe za Coco Beach Aprili 23,2022 ikiwa ni katika raundi ya 11 ya ligi hiyo ambayo inahusisha takribani timu 13.

Akizungumza na waandishi wa habari za michezo kwenye mkutano uliofanyika makao makuu ya TFF Mratibu wa Ligi hiyo Boniface Pawasa ambaye pia ni Kocha wa timu ya Taifa Soka la Ufukweni alisema kuwa mwishoni mwa wiki hii zitachezwa mechi 6 za kundi A na B zote kwenye fukwe za Coco.

“Zitachezwa mechi 3 za kundi A jumamosi Aprili 23 kutakuwa na mtanange kati ya Ilala FC vs Savannah Boys zote kutoka manispaa ya Ilala, Friends Rangers watacheza na PCM Buza na mchezo wa mwisho utakao chezwa majira ya saa 11 jioni utawakutanisha kati ya DSM Football Center vs Vingunguti Kwanza. Mechi zitaanza saa 9 alasiri mpaka majira ya saa 11 jioni”.

Alisema pia mechi za kundi B zenyewe zitachezwa Jumapili ya Aprili 24 kwenye fukwe hizo ambapo mchezo wa kwanza utakuwa ni kati ya K’nyama Sand Heroes Vs Msasani Mabingwa, mchezo ata utawakutanisha Mburahati FC vs Kisa FC na mchezo wa mwisho wataminyana Friends of Mkwajuni vs Mshikamano.

Kocha Pawasa alieleza kuwa lengo hasa la ligi hiyo ni pamoja na kuunda timu ya Taifa ya Soka la Ufukweni ambapo kwa mwaka huu timu hiyo inatarajia kushiriki mashindano ya Beach Soccar Africa Cup of Nation (BAFCON) mashindano yanayotarajiwa kufanyika mwezi Oktoba mwaka huu huko jijini Maputo nchini Msumbiji.

Aidha kocha huyo akiendelea kutaja mipango ya timu hiyo wanayo tarajia kuiunda mara baada ya kuisha kwa Ligi alisema kuwa kabla ya mwezi Oktoba timu hiyo ya Taifa itakuwa na mechi moja ya kufuzu kushiriki mashindano hayo ya BAFCON inayo tarajiwa kuchezwa mwezi Julai mwaka huu.

Mwishoni mwa wiki ijayo Ligi kuu ya Soka la Ufukweni itaendelea pia kwa kupigwa mechi za mzunguko wa pili kutoka mwisho na baadaye kumalizia mzunguko wa tatu amba ndio wa mwisho utakao toa timu nne kila kundi, timu zitakazo cheza kwenye hatua ya Robo Fainali mpaka kwenye hatua nyingine za kumtafuta Bingwa kwa msimu huu.