Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mh. Job Ndugai leo ametembelea Kambi ya Timu ya Taifa “Taifa Stars” iliyopo Cairo,Misri kujiandaa na mashindano ya AFCON yanayotarajia kuanza Juni 21, 2019.
Spika Ndugai alipata fursa ya kuzungumza na wachezaji akiwa na ujumbe kutoka kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Dkt.John Pombe Magufuli, ambaye amewataka Wachezaji kujituma na kupeperusha vyema Bendera ya Tanzania.
“Naomba kila mmoja wenu ajue kwamba mmebeba jukumu zito, nimekuja kama Spika lakini namuwakilisha Mh. Rais Magufuli, nimewaletea salamu zake mwenyewe, anawasalimia sana, anawafuatilia kwa karibu sana na mechi zenu zote atakua anazifuatilia kwa ukaribu sana,anawatakia Kila la kheri kwenye michuano hii mikubwa Barani Afrika, ujumbe wangu ndo huo kutoka kwa Mh. Rais John Pombe Magufuli” ,amesema Spika Ndugai.
Taifa Stars ipo Kundi moja na Algeria,Senegal na Kenya na itaanza kutupa karata yake ya Kwanza dhidi ya Senegal Juni 23,2019.