Stars Bado Inanafasi Kufuzu Hatua Inayofuata
Kocha Mkuu wa kikosi cha timu ya Taifa ya Tanzania “Taifa Stars” Kim Poulsen amesema kuwa Stars bado inanafasi ya kupambana kuhakikisha inafuzu hatua ya makundi na kusonga kwenye hatua nyingine inayofuata katika mashindano ya kufuzu kushiriki michuano mikubwa ya Kombe la Dunia hapo mwakani.
Hayo aliyasema mara baada ya kumalizika kwa mchezo kati ya Taifa Stars na Benin, uliopigwa Oktoba 07, 2021 katika dimba la Mkapa Jijini Dar es Salaam ambapo timu hiyo haikuweza kupata alama kwenye mchezo huo iliporuhusu kufungwa bao moja kwa sifuri; bao hilo likifungwa na mchezaji aitwae Mounie Steve jezi namba (9) mnamo dakika ya 71.
Kocha Poulsen alisema kuwa kikosi chake kimecheza vizuri licha ya kutopata matokeo kikiwa katika uwanja wa nyumbani huku akidai kuwa bado kikosi hicho kinayo nafasi ya kupambana na kupata ushindi ugenini pia. Kocha huyo aliendelea kueleza kuwa mchezo wa mpira wa miguu ni mchezo wa makosa na kutengeza nafasi na kuzitumia kikamilifu nafasi hizo; Stars walitengeneza nafasi za magoli kadhaa lakini hawakuweza kuzibadilisha na kuwa magoli, hivyo endapo watazitumia nafasi watakazozipata vyema nafasi ya kusonga mbele ipo.
Aidha, kocha Poulsen aliongeza kuwa timu ya Benin ni nzuri inauwezo mzuri huku akisema kuwa lolote linawezekana kwa kuwa mchezo wa mpira wa miguu ni wa makosa na nafasi; hivyo, yeyote atakayefanikiwa kutengeneza nafasi na akazitumia vyema anaweza kuibuka mshindi.
Naye mchambuzi wa soka na mchezaji wa zamani wa Stars Douglas Muhani alisema kuwa endapo kikosi hicho cha Taifa “Taifa Stars” kitarekebisha baadhi ya makosa madogo madogo na kuongeza jitahada zaidi za kupambana bado kinaweza badili matokeo hayo na kupata alama tatu kwenye mchezo wake wa marudiano wa Oktoba 10 huko Benin.
Mbali na mchezo huo wa Stars na Benin, katika mchezo mwingine wa kundi “J” Congo DR ilishuka dimbani ikiwakaribisha Madagascar mchezo huo ukipigwa majira ya saa kumi jioni ambapo mwenyeji Congo alifanikiwa kuibuka na ushindi wa bao mbili kwa sifuri na kufanikiwa kufikisha alama 5 ikiwa alama mbili pungufu nyuma ya Benin mwenye jumla ya alama saba baada ya kucheza michezo yao mitatu huku Tanzania wakisalia na alama zao nne na Madagascar wao wakibuluza mkia kwenye kundi hilo.
Magoli yaliyopatikana kwa Congo yalipachikwa kimiani na wachezaji; C. Akolo dakika 35 na D. Mbokani aliyepigilia msumari wa mwisho kunako dakika ya 79 ya mchezo huo na kuufanya mchezo huo kutamatika huku ubao ukisoma 2-0. Michezo ya marudiano kati ya Tanzania na Benin itapigwa Oktoba 10 2021 huko Benin huku Congo wao wakiwafuata Madagascar.