Stars” Hesabu Kali Dhidi ya Mongolia
Kikosi cha timu ya Taifa ya Tanzania “Taifa Stars” kilichopo Azerbaijan kwaajili ya michezo miwili ya kirafiki “FIFA Series 2024” kimeendelea na hesabu za kuuendea mchezo wake wa pili na wa mwisho dhidi ya Mongolia utakao chezwa Machi 25, 2024 majira ya saa 10:00 za jioni.
Mikakati hiyo mikali imeelezwa na kaimu kocha mkuu wa timu hiyo Hemedi Suleiman akizungumzia maandalizi yao, kocha alisema hawakufurahishwa na matokeo ya mchezo wa kwanza dhidi ya Bulgaria hivyo wamefanyia kazi mapungufu yote na kuhakikisha hayatojirudia kwenye mchezo unaofuata.
Aidha alisema Mongolia ni timu nzuri, hivyo wamejipanga kupambana zaidi kwenye mchezo huo kuhakikisha wanapata matokeo mazuri dhidi yao
“Mongolia tumewaona kwenye mchezo dhidi ya Azerbaijan wanacheza vizuri na sisi tutakuwa makini zaidi kwasababu tunahitaji kushinda, sipo tayari kuona tunapoteza michezo yote miwili” alisema kocha.
Sambamba na hayo Kwa upande wa wachezaji naye Feisal Salum Kwa niaba ya wachezaji aliahidi kupambana zaidi wao kama wachezaji baada ya kupokea maelekezo kwenye uwanja wa mazoezi na kwamba watarekebisha changamoto zote na kuhakikisha watatumia vizuri nafasi watakazozipata ili waweze kushinda.
Ikumbukwe kabla ya mchezo huo Stars ilipoteza kwenye mchezo wa kwanza FIFA Series dhidi ya Bulgaria Kwa goli 1-0. Hivyo wamesaliwa na kibarua cha kuwakabili Mongolia katika kukamilisha hesabu za mashindano hayo mapya kabisa yaliyo pitishwa kwenye kikao cha 73 cha Shirikisho la Mpira wa Miguu Duniani FIFA.