Stars Mguu Sawa Kuelekea Kombe la Dunia Qutar 2022

Kocha wa timu ya Taifa Tanzania, ‘Taifa Stars’ Kim Poulsen atangaza kikos kitakacho vaana na DR Congo Septemba 2, mwaka huu huko nchini Congo kabla ya kurudiana mnamo tarehe 7 mwezi huo huo.

Kikosi hicho cha Stars kimeitwa rasmi kuanza kambi ifikapo tarehe Agosti 25 kwa ajili ya kujinoa tayari kwenda kuiwakilisha nchi katika michezo miwili ya kufuzu kushiriki michuano mikubwa ya Kombe la Dunia mwaka 2022 itakayofanyika Qutar.

Akizungumza na waandishi wa habari za michezo kwenye 19 Agosti, 2021 yalipo Makao Makuu ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania, kocha Kim Poulsen alisema kuwa amejitahidi kuchanganya wachezaji wa kada zote huku akiwapa nafasi zaidi vijana ili nao waweze kukua na kuendelea kupata uzoefu zaidi kwa ajili ya kujitengenezea akiba nzuri ya baadaye.

Kocha Kim alisema kuwa alitamani sana kuanza kambi mapema kuanzia taraehe 15 Agosti lakini kutokana na sababu mbalimbali zilizojitokeza zimempelekea yeye kutangaza kikosi hicho sasa na kuwaita wachezaji hao kufika kambini tarehe 25 Agosti 2021. Kambi itakayochukua takribani siku 5 kabla ya kuondoka kuelekea Congo DR kwa ajili ya kuvaana na timu hiyo kwenye mchezo wa awali utakaopigwa katika dimba la TP Mazembe, Lumumbashi.

Aidha kocha Poulsen aliongeza kuwa katika kuhakikisha kikosi kinakuwa tayari na ili kufahamu ni kwa namna gani wachezaji wake wanaelewa na kushika maelekezo yanayotolewa na benchi la ufundi la Stars anatarajia kupata mechi moja ya kimataifa ya kirafiki ambayo itachezwa tarehe 28 Agosti mwaka huu na baada ya mchezo huo timu itakuwa tayari kuelekea Congo DR kwa ajili ya mchezo wao wa ugenini wa makundi ya kufuzu kushiriki Kombe la Dunia 2022.

Kocha Poulsen alidai kuwa uteuzi wa majina ya wachezaji wanaounda timu hiyo ya Stars umezingatia zaidi wachezaji wanaoshiriki Ligi Kuu ya Vodacom ambao walionesha uwezo mkubwa kwenye ligi  na wenye uzoefu mkubwa pia, licha ya kuwepo kwa baadhi ya maingizo mapya machache chilia mbali wale wanaocheza ligi za nje ya nchi kama akina Mbwana Ali Samatta.

Majina ya wachezaji 28 wanaounda kikosi kilichotajwa na kocha Poulsen ni: magoli-kipa; Aishi Salum Manula (Simba SC), Ramadhani Kabwili (Young Africans SC),  Metacha Mnata(   ) na Wilbol Maseke (Azam FC). Wachezaji wa ndani ni; Shomari Kapombe (Simba), Israel Mwenda (Simba), Erasto Nyoni (Simba), Dickson Job (Young Africans),  Bakari Mwanyeto (Young Africans), Kennedy Juma (Simba), Lusajo Mwaikenda (Azam FC), Abdulrazack Mohammed (Azam FC), Mohammed Hussein (Simba), Nickson Kibabage ( Youssoufia FC Morocco) na Edward Charles Manyama kutoka Azam FC.

Wachezaji wengine ni pamoja na; Ayoub Lyanga (Azam FC), Meshack Mwamita (Gwambina FC), Novatus Dismas (Maccabi Tel Aviv-Israel), Mzamiru Yassin (Simba), Mudathir Yahya Abbas (Azam FC),  Feisal Salum (Young Africans),  Salum Abubakar (Azam FC),  Zawadi Mauya (Young Africans), Iddy Seleman (Azam FC), Abdul Hamis Suleiman (Coastal Union), Mbwana Samatta (Fenerbahce-Uturuki), John Bocco (Simba) na Simon Msuva anayechezea timu ya Wydad AC-Morocco.

Kwa mujibu wa maelezo ya kocha Mkuu wa Taifa Stars Kim Poulsen ni kwamba timu hiyo ya Taifa inatarajia kucheza michezo sita ambapo michezo minne ya kufuzu itachezwa mwaka huu ikianza na miwili itakayochezwa tarehe 2 na ule wa marudiano utakaochezwa 7 Septemba na michezo miwili ikitarajiwa kuchezwa Oktoba, 2021 huku miwili mingine ikitarajiwa kuchezwa mwanzoni mwa mwaka 2022.

Endapo Stars ikifanikiwa kufanya vema katika michezo hiyo yote inaweza kusonga mbele na hatimaye kufanikiwa kushiriki michuano ya Kombe la Dunia huko Qutar mwakani.