Stars tayari kwa Mchezo wa Marudiano

Timu ya Taifa ya Tanzania Taifa Stars ipo tayari kukipiga kwenye mchezo wa marudiano dhidi ya Somalia, baada ya kuanza kwa ushindi kwenye mchezo wa awali uliochezwa Julai 23, 2022 kwenye dimba la Benjamin Mkapa.

Stars inatarajia kwenda kuzichanga karata zake kwenye mchezo huo wa marudiano Julai 30, 2022 majira ya saa 10:00 za jioni wakiwa na lengo kubwa la kuendeleza kupata matokeo chanya ili kujihakikishia Zaidi kufuzu kwenye michuana hiyo ya CHAN.

Akizungumza na waandishi wa habari za michezo kocha mkuu Kim Poulsen alisema kuwa wachezaji wote wapo tayari kwaajili ya mechi isipokuwa Aishi Manula ambaye alipata majeraha kwenye mechi ya awali. Hata hivyo kocha aliongeza kuwa ni mchezaji mmoja aliye ongezeka kwenye kikosi Daniel Lyanga ambaye hakuwa kwenye kikosi huku David Luhende akirejea kwenye kikosi baada ya kutoka kwenye majeruhi.

Kwa upande wa nahodha wa kikosi hiko mlinda mlango Aishi Manula amesema wenyewe kama wachezaji wako tayari kwaajili ya mchezo na malengo yao ni kupata matokeo mazuri Zaidi ya waliyopata kwenye mechi ya awali na kwamba wamekwishakuyajua madhaifu na ubora wa wapinzani wao hivyo wamejiandaa kulinda na kwenda kushambulia kwenye mchezo huo.

Kuelekea katika mchezo huo TFF imewataka mashabiki na wadau wa soka kuweza kujitokeza kwa wingi kwenye mechi hiyo kuwapa sapoti Taifa Stars, huku wakitangaza na viingilio kuwa ni 5000 VIP na 2000 kwa Mzunguko.