Stars Yainyong’onyeza Malawi Kwa Mkapa

Mchezo wa kirafiki kati  ya Taifa Stars na Malawi (Miale ya Moto) umemalizika kwa timu ya taifa ya Tanzania kuibuka na ushindi wa bao mbili kwa sifuri.

Mchezo huo uliopigwa majira ya saa 10:00 jioni katika uwanja wa Mkapa jijini Dar es Salaam ulionekana kutokuzaa matunda kwa timu zote kwenye kipindi cha kwanza na badala yake katika kipindi cha pili timu zote zikaamua kubadili mbinu zake. Malawi waliingia na mbinu ya kushambulia zaidi mara baada ya kukisoma kikosi cha Stars, wakati kocha wa Stars Kim Poulsen aling’amua mbinu yao na kuamua kufanya mabadiriko akiwatoa; Mudathir Yahya, Shomari Kapombe, Salum Abubakar, Erasto Nyoni, Yusuph Mihiru na kuingia Israel Mwenda, Kibu Denisi, Mzamiru Yassin, Ayubu Lyanga na Abdul Hamisi.

Mabadiliko hayo yalileta mafanikio kwa upande wa Stars ambapo kunako dakika ya 67 ilifanikiwa kupata bao la kuongoza kupitia kwa mshambuliaji John Bocco, huku bao la pili likipachikwa na Israel Mwenda mnamo dakika ya 74 na kuufanya mchezo huo kumalizika kwa Stars kutoka kifua mbele kwa bao 2-0.

Kocha wa Stars, Kim Poulsen alisema kuwa kwanza amefarajika  kwa matokeo hayo ya ushindi na kwamba anawapongeza wachezaji wake huku akidai kuwa mabadiliko aliyoyafanya katika kipindi cha pili yalileta faida. Kocha Kim aliongeza kuwa ushindi huo umetokana na nidhamu na ushirikiano baina ya wachezaji ambao hawakujali ukubwa na udogo wa mchezaji. Hata hivyo, kocha Kim alisema anahitaji  michezo ya kirafiki mingi zaidi ili kuboresha kikosi chake kutoka kwenye ngazi ya kitaifa na kwenda ngazi ya kimataifa.

Kwa upande wa kocha wa timu ya Malawi Bob Gerald yeye aliwashukuru watanzania kwa kuwapatia nafasi ya kucheza nao na kwamba wamejifunza mengi ambayo watakwenda kuyafanyia kazi. Kocha huyo aliongeza kuwa timu yake ilikuwa ikipiga pasi nyingi katika kipindi cha kwanza lakini kwenye kipindi cha pili walionekana kupoteza umakini uliopelekea  Stars kuweza kutengeneza nafasi nyingi zilizowapatia ushindi.