STARS YAPAA KUIFUATA EQUATORIAL GUINEA
Kikosi cha Wachezaji 30 wa Timu ya Taifa “Taifa Stars” kimeondoka jijini Nairobi, Kenya kwenda Malabo, Equatorial Guinea kwa ajili ya mechi ya mchujo ya AFCON dhidi ya wenyeji itakayofanyika Alhamisi, Machi 25 mwaka huu.
Taifa Stars ilipiga Kambi Nairobi ambako ilicheza mchezo mmoja wa kirafiki wa kimataifa na Kenya “Harambee Stars” na kupoteza kwa mabao 2-1 bao la Stars likifungwa na Ayoub Lyanga.
Kikosi hicho kinaondoka kikiwa kamili huku nahodha Mbwana Samatta,Simon Msuva na Yohana Mkomola wakiongeza nguvu baada ya kujiunga na kambi.
Kocha mkuu Kim Poulsen amesema wamefanya maandalizi mazuri kuikabili Equatorial Guinea na baadaye Libya japo anaamini haitakuwa kazi rahisi.
Poulsen ameongeza kuwa, kila mmoja nia yake ni kufanya vizuri ili kuikata tiketi ya kucheza AFCON jambo ambalo ni matamanio ya kila mchezaji.
Naye nahodha wa kikosi hicho Mbwana Samatta amesema wanakwenda katika mchezo huo wakiuchukulia kama fainali ya kufuzu AFCON na wanajua utakuwa mgumu kwa kuwa wapinzani wao watakuwa nyumbani na watafanya kila jitihada kupata matokeo.
Samatta ameongeza kuwa wamefanya maandalizi mazuri na wanakwenda kushindana kuhakikisha wanaibuka na ushindi utakaowaweka kwenye nafasi nzuri ya kuikata tiketi ya kufuzu.
Wachezaji walioondoka ni Aishi Manula, Metacha Mnata, Juma Kaseja, Shomari Kapombe, Israel Mwenda, Erasto Nyoni, Bakari Nondo, Kelvin Yondani, Kennedy Juma, Laurent Alfred, Mohammed Hussein, Nickson Kibabage, Yassin Mustapha, Hassan Dilunga, Mzamiru Yassin, Jonas Mkude, Feisal Salum, Himid Mao, Salum Abubakar, Farid Mussa, Iddy Nado, Thomas Ulimwengu, John Bocco, Shaban Chilunda, Deus Kaseke, Abdul Hamis, Ayubu Lyanga, Yohana Mkomola, Simon Msuva na nahodha Mbwana Samatta.