Stars Yawasili Dar na Kupokea Kitita cha Goli la Mama
Timu ya Taifa ya Tanzania ” Taifa Stars” imerejea nchini Juni 13, 2024 na kukabidhiwa kitita cha milioni Kumi (10,000,000/=) za Goli la Mama mara baada ya kuwasili kwenye uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Kambarage Nyerere.
Kikosi hicho kiliwasili nchini kilitokea Ndola Zambia ambako kilienda kusaka tiketi ya kufuzu Kombe la Dunia 2026 dhidi ya Zambia ambapo katika mchezo wake kilifanikiwa kupata ushindi wa bao 1-0 kikiwa kwenye ardhi ya ugeni Ndola.
Mchezo huo wa tatu katika harakati za kuwania kufuzu michuano hiyo ya Kombe la Dunia ulikuwa mgumu kwa pande zote licha ya Taifa Stars kufanikiwa kuibuka na ushindi huo wa bao 1-0 bado haikuwa rahisi kwao kupata matokeo hayo.
Katika mchezo huo, Stars iliandika bao lake mapema kipindi cha kwanza kunako dakika ya 05 kupitia kwa Waziri Junior aliyepokea pasi safi kutoka kwa Mudathir Yahya Abbas aliyepoka Mpira kutoka kwa kiungo mkabaji wa Zambia.
Akikabidhi fedha hizo za Goli la Mama na mfano wa hundi ya shilingi milioni mia moja (100,000,000/=) Waziri wa Wizara ya Utamaduni Sanaa na Michezo Dkt. Damas Ndumbaro alisema kuwa fedha ya Goli la Mama hailali na kwamba hukabidhiwa mara baada ya mchezo, na kwamba wameamua kuwakabidhi fedha hiyo uwanjani hapo ikiwa ni kawaida ya utaratibu ambao umekuwa ukufabyika siku zote.
Kaimu Kocha Mkuu wa “Taifa Stars” Hemed Morocco akiwa katika uwanja huo wa Ndege wa Julius Nyerere aliwapongeza wachezaji wake kwa kujituma na kupata ushindi huo huku akiwashujuru Watanzania wote waliokuwa bega kwa bega Kila wakati. Huku pia akitoa Shukrani kwa Serikali ya Awamu ya Sita kwa kuendelea kutoa sapoti kwa akisema kufanya hivyo kumewaongezea ari na morali ya kupambana zaidi wachezaji wote.
Naye Himid Mao Mkami Kwa niaba ya wachezaji wenzake alimshukuru Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan na Serikali kwa ujumla kutokana na hamasa ambayo amekuwa akiitoa kwao wakisema hakika bonasi anazozitoa kwao zimekuwa ni chachu ya Mafanikio kwani ushindi waliouoata ugenini ulichangiwa pia na ahadi ya Serikali.
Kikosi hicho kiliwasili uwanjani hapo majira ya saa 12 jioni huku kikiambatana na viongozi mbalimbali waliokuwa katika msafara huo na kikipokelewa na wadau wa soka nchini wakiwemo viongozi wa Serikali na TFF pia.