Steven Mnguto: Makocha Jiongezeni

Mwenyekiti wa bodi ya ligi (TPLB) na Makamu wa pili wa Rais wa  TFF  Steven Mnguto amewataka makocha kujiongeza zaidi katika upande wa lugha na elimu ya mpira ambayo inazidi kubadilika kila uchao jambo ambalo litakuwa msaada mkubwa kwao katika kupata ajira za ndani na zile za nje ambao wengi wanazikosa kwa kutokukidhi vigezo hivyo viwili.

Hayo aliyasema wakati anafungua rasmi kozi ya Ukocha CAF-Diploma C iliyokuwa inafanyika yalipo Makao Makuu ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF); kozi hiyo iliyojumuisha washiriki 30 kutoka katika mikoa mbalimbali ya Tanzania.

Mnguto aliendelea kuwasisitiza makocha juu ya  ufanyaji kazi kwa weledi na kuzingatia sheria na  kanuni zilizowekwa na kuacha kufanya kazi kwa hofu na kujaribu kufurahisha kila mtu huku soka likiendelea kuzorota kutokana na makosa ya watu wachache, hivyo aliwataka washiriki waliopata nafasi hiyo wakasimamie misingi ya sheria, kanuni na taratibu za soka.

Naye mkufunzi wa kozi hiyo ambaye pia ni Mkurugenzi wa ufundi Oscar Mirambo  alisema; “tutaendelea kutekeleza mpango mkakati uliowekwa na TFF wa kuhakikisha Tanzania inakuwa kitovu cha maendeleo ya soka katika nyanja zote ikiwa ni pamoja na kuwaendeleza makocha wetu ili waweze kuwa na elimu stahiki ya kufundisha wachezaji lakini pia waamuzi na kada nyinginezo, hivyo mafunzo haya yatakuwa endelevu na kuhakikisha yanawafikia walengwa sehemu mbalimbali.” Alisema Mkurungezi Mirambo.

Kwa kutambua umuhimu mkubwa wa kozi hiyo TFF ilimualika Mkufunzi kutoka CAF Hanour Janza ili kuweza kuwashirikisha washiriki hao uzoefu wake katika tasnia ya ukufunzi wa mchezo wa Mpira wa miguu ambapo Janza aliwaasa makocha hao kuchukulia mafunzo hayo  kwa ukubwa na kuhakikisha wanazingatia na kujitahidi kendelea kuongeza elimu kila wanapopata nafasi kwani takwimu zinaonyesha kwa Afrika ni makocha 10 pekee ambao wana elimu ngazi ya juu ya ukocha (PRO licence). Hii inatoa taswira ya nanma gani uhitaji wa makocha ulivyo mkubwa.

Akizungumza kwa niaba ya washiriki wenzake Anna Mathias (kocha wa magolikipa Simba Qeens) ambaye ni mshiriki pekee wa kike katika kozi hiyo aliushukuru uongozi wa TFF katika kuhakikisha linaendelea kuwajengea uwezo makocha  ili waweze kufanya kazi zao kiueledi, huku akitoa rai kwa wanawake kujitokeza kwa wingi kushiriki mafunzo mbalimbali na kujikita katika tasnia ya michezo ambayo imekuwa ikitoa fursa ya ajira kwa watu wengi.

Washiriki wa kozi ya ukocha Caf Diploma C ni pamoja na Khalid J. Ngome, Kisavery F. Kitambara , Rajab  yusufu, Beatus Michael, Norbert D. missana, Mximilian Marcus, Ally Ruvu Kiwanga, Anna M. Joel, Ally Kamwe, Dickens E. Somaili, Catis H.Tully, Henry Sempa, Methusela N. Johnson, Imani N. Mwalupetelo, Lucas A. Mhindi, Hussein A. Bunu, Shaibu Sanatu, Geofrey Mhando, Adam Ali Simai Agrey M. Ambros, Buberwa  D. Bilikesi, Shauri I. Mussa, Saidi A. Achimwene, Alex E. Lusekelo, Remigius K. Felcian, Rtta A. Tiba, Adam S. Mbwana, John Mashaka, Francis Mkanula na Mwalimu Chalamila.