Taifa Stars Kuvaana na Sudan kwa Mkapa
Timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ inatarajia kushuka dimbani hapo kesho (Machi 29, 2022) kuikabili timu ya Taifa ya Sudan kwenye mchezo utakao pigwa majira ya saa 1:00 usiku katika uwanja wa Benjamin Mkapa, Jijini Dar es Salaam.
Mchezo huo wa kirafiki wa kimataifa utapigwa hiyo kesho ikiwa ni muendelezo wa michezo ya kalenda ya FIFA ambapo mchezo wa kwanza uliopigwa kwa Mkapa Machi 23, 2022 ukiwakutanisha Taifa Stars dhidi ya Afrika ya Kati ambapo Stars ilishindi kwa bao 3-1.
Akizungumza na waandishi wa habari kuelekea mchezo huo, kocha wa kikosi cha Taifa Stars, Kim Poulsen alisema kuwa kikosi chake kimeendelea na maaandalizi yake vyema akidai kuwa mara tu baada ya mchezo wa kwanza dhidi ya Afrika ya Kati kumalizika timu hiyo iliendelea kujifua kwa ajili ya mchezo unaofuata ambao ni muhimu kwa kikosi hicho kujipima nguvu ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya michuano ya AFCON na CHAN inayotarajia kufanyika Mwezi Juni na Julai mwaka huu.
Aidha, kocha Kim aliezea kuhusu hali ya wachezaji wake akisema kuwa kiungo wa Stars na klabu ya Young Africans Feisal Salum(Fei toto) ataukosa mchezo huo dhid ya Sudan kutokana na majeruhi ya msuli aliyoyapata huku daktari wa timu ya Taifa Lisobine Kisongo alithibitisha hilo na kusema kuwa kiungo huyo anaweza kukaa benchi kwa takribani wiki sita.
Daktari Kisongo alifafanua kwamba uchunguzi wa kitabibu umebaini kuwa Fei toto aliumia akiwa na klabu yake muda mrefu japokuwa yeye mwenyewe aliendelea kucheza kama kawaida jambo ambalo Dkt. Kisongo anasema ni hatari kwa afya ya mchezaji, kwa kipaji chake, timu yake na taifa pia; kwani kwa mujibu wa taratibu za Kitaabibu mchezaji anapoumia anatakiwa kupumzika ili kuruhusu matibabu ya kina kufanyika kwa utulivu zaidi; kuendelea kumchezesha kunaweza hatarisha zaidi afya ya mchezaji na hivyo kuweza hata kumfanya kushindwa kucheza mpira au kushuka kiwango chake.
Katika hatua nyingine Kocha Kim alitanabaisha kwamba kwenye mchezo wa Stars dhidi ya Sudan kikosi kitakuwa na mabadiliko makubwa huku akidai kuwapatia nafasi kubwa zaidi vijana, wakati huo huo alisema wachezaji wa klabu ya Simba SC wao amewapatia ruhusa kwenda kujiandaa na mchezo wao wa Kimataifa wa Kombe la Shirikisho Afrika, unaotarajiwa kuchezwa Aprili 3, 2022 kwa Mkapa.