Timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ imeondoka rasmi leo tarehe 11 Novemba, 2020 ikitokea Uturuki ilipokuwa imepiga kambi na kuelekea nchini Tunisia kwa ajili ya mchezo wake dhidi ya timu Tunisia, mchezo unaotarajiwa kuchezwa siku ya Ijumaa ya tarehe 14 Novemba 2020.
Akiongea kutoka uwanja wa ndege wa Instanbul-Uturuki, Kocha Mkuu wa Taifa Stars Etienne Ndayiragije amesema kwamba tangu wafike Uturuki maandalizi yote yako vizuri na kikosi chake kimejiandaa vizuri kwa kufanya mazoezi ya kutosha kwani mpaka hivi sasa hakuna majeruhi yoyote huku akieleza kuwa wachezaji wote wana hamasa kubwa ya mchezo huo na wameahidi kuonesha kitu cha tofauti katika mechi hiyo.
Aidha Kocha huyo alizungumzia pia kuhusu kukosekana kwa nahodha wa ‘Taifa Stars’ Mbwana Ali Samatta kutokana na kupata majereha katika mechi yake ya mwisho akiwa na timu yake ya Fenerbache Sk, na kwa mujibu wa madaktari wake walishauri kuwa anapaswa kupata mapumziko ya muda wa wiki mbili. Hivyo basi kutokana na ushauri huo wa madaktari, Samatta atakosekana pia hata katika mechi ya marudiano inayotarajiwa kuchezwa nyumbani (Tanzania) mnamo tareha 17 Novemba, 2020.
Kocha Ndayiragije amesisitiza kwamba licha ya kukosekana kwa Samatta bado kikosi chake kitafanya vizuri kwani ni kikosi bora kilichojiandaa vizuri na kitapambana kuhakikisha kinapata matokeo mazuri na kuletea sifa nzuri kwa Taifa la Tanzania, hivyo watanzania wote wawe na imani na timu yao na kwamba haitawaangusha.