Taifa Stars Sudan Ngoma Ngumu

Mchezo wa kirafika wa Kimataifa uliopigwa kwa Mkapa, Machi 29, 2022 uliwakutanisha Taifa Stars dhidi ya Sudan na kumalizika kwa timu hizo kutoshana nguvu baada ya kutoka sare ya bao moja kwa moja.

Mchezo huo uliopigwa majira ya saa 1:00 usiku ulikuwa ni wa pili kwa timu zote ambapo Stars katika mchezo wake wa kwanza ilikutana na Jamhuri ya Afrika ya Kati ikaiadhibu kwa jumla ya mabao 3-1 huku Sudan wao wakipata suluhu tasa.

Mechi hiyo ya pili katika timu, ilikuwa ngumu kwani timu zote zilikuwa zimesomana kufuatia kila timu kushuhudia mbinu za mwenzake mara baada ya kushudia aina ya mchezo inayocheza timu pinzani kwenye mchezo wake wa kwanza.

Sudan ndio ilikuwa ya kwanza kuandika bao la kuongoza lililofungwa dakika ya 2 na mchezaji jezi namaba 10, aitwae Siddig Toto aliyeunganisha mpira uliopanguliwa na Metacha Mnata baada ya mchezaji wa Sudan kuachia kobora kali. Bao hilo la Sudan lilidumu mpaka kipindi cha kwanza kinamalizika.

Kipindi cha pili kilianza kwa presha zaidi kwa upande wa Taifa Stars mara baada ya kuwa nyuma kwa bao moja ikamua kusaka bao la kusawazisha kwa udi na uvumba; hali iliyopelekea kusawazisha bao hilo kunako dakika ya 68 ya mchezo kupitia mshambuliaji wa kimataifa Saimon Msuva aliyeunganisha mpira ulipigwa kwa gamba na George Mpole.

Akiongea na waandishi wa habari kocha wa Taifa Stars Kim Poulsen alisema kuwa kikosi chake kilicheza vizuri licha ya kuwepo kwa makosa madogomadogo ambayo yameendelea kujitokeza kwa baadhi ya nyota wake. Hata hivyo, Kim alisema kuwa mchezo huo umesaidia kuwapima wachezaji na kubaini makosa ili yeye pamoja na benchi la ufundi liweze kuyafanyia kazi kwa ajili ya kujiweka sawa kwa michuano ijayo ya CHAN na AFCON mwaka huu.

Kwa upande wa kocha wa Sudan Bulhan El- Tia yeye alisema kuwa lengo la mchezo hiyo miwili sio kupata matokeo bali ni kuzipima timu na kufahamu makosa au upungufu uliopo katika kikosi chake ili aweze kukifanyia marekebisho kabla ya kuingia kwenye michuano ijayo. Kocha huyo hakusita kukipongeza kikosi chake kwa kuonesha uwezo mkubwa huku akikipongeza pia kikosi cha Stars.

Mchezo uliopigwa Machi 29, 2022 ulikuwa wa kukamilisha ratiba ya mechi mbili kwa kila timu ambapo Stars na Sudan zote zilianza kwa kukutana na Jamhuri ya Afrika ya Kati; michezo hiyo ya kirafiki ya Kimataifa ni ya kalenda ya FIFA.