Taifa Stars yabeba alama tatu dhidi ya Uganda

Timu ya taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ imebeba alama tatu dhidi ya timu ya Taifa ya Uganda ‘The Cranes’ baada ya kupata ushindi wa goli 1-0 katika mchezo wa kufuzu AFCON uliopigwa majira ya saa 11:00 jioni katika uwanja wa Suez Canal, Misri.

Goli pekee la ushindi lilifungwa na Simon Msuva katika dakika ya 68 akimalizia pasi nzuri iliyotolewa na Dickson Job. Taifa Stars iliendelea kuongoza kwa goli moja hadi dakika 90 zinatamatika licha ya Uganda kufanya mabadiliko kadhaa ambayo hayakuzaa matunda na hivyo kuwa mwanzo mzuri Kwa kocha mpya wa Taifa Stars Adel Amorouche.

Akizungumza baada ya Mchezo kumalizika kocha wa Taifa Stars alisema sijawahi kujiandaa kutoa Sare wala kupoteza katika mchezo siku zote najiandaa Kwa ajili ya kushinda, Niko hapa kwa ajili ya kuishinda hii timu, kuleta mabadiliko na kubadili mtazamo.

“Kuna watu wamefanya Kazi nyuma yangu niko hapa kwa ajili ya kuendeleza na kuongeza vitu vipya, wachezaji wakiendelea kujitoa pamoja na mashabiki kujitokeza kwa wingi katika uwanja wa nyumbani itakuwa furaha yangu kubwa” alisema Kocha Amorouche.

Kwa matokeo hayo taifa stars inafikisha alama nne na kusogea katika nafasi ya pili nyuma ya Algeria yenye alama tisa ambaye ni kinara wa kundi F wakati Niger ikishika nafasi ya tatu kwa alama 2 na Uganda ikiburuza mkia Kwa alama moja baada ya timu zote kucheza michezo mitatu.

Mchezo wa marudiano Kati ya Taifa Stars dhidi ya Uganda utachezwa Machi 28,2023 katika uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam.