Taifa Stars Yafuzu AFCON Mbele ya Miamba Algeria, Yavuna  Milioni 500 za Samia

Timu ya Taifa ya Tanzania “Taifa Stars” imefanikiwa kufuzu kushiriki Michuano Mikubwa ya AFCON baada ya kuitunishia misuli timu ya Taifa ya Algeria katika mchezo uliopigwa Agosti 7, 2023 nchini Algeria ambapo Stars ilivuna alama moja muhimu iliyoipatia fursa ya kushika nafasi ya pili kwenye kundi F ikifikisha alama 8, alama moja mbele ya majirani zao Uganda waliofikisha alama 7 na kushika nafasi ya tatu katika kundi hilo.

Mchezo huo uliokuwa ukisubiriwa na wadau wengi wa soka ndani na nje ya nchi ulipigwa majira ya saa 2:00 usiku kwa Algeria SAWA na saa 4:00 usiku kwa saa za Afrika Mashariki ulikuwa wa kimbinu zaidi ambapo timu ya Taifa Stars ilikuwa na jukumu Moja tu kuhakikisha inatafuta alama moja pekee Kwa udi na uvumba; jambo ambalo kimbinu lilifanikiwa chini ya Kocha Mkuu Adel Amrouche anayekiongoza kikosi hicho kilichobeba matumaini makubwa ya Watanzania.

Kufuzu kwa timu ya Stars kumeifanya timu hiyo kuvuna Milioni Mia Tano (500,000,000) za za Kitanzania kutoka kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye kabla ya mchezo huo akiahidi kutoa kiasi hicho cha fedha mara timu hiyo itakapofanikiwa kufuzu kucheza Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2024 nchini Ivory Coast.

Akizungumza na wachezaji na viongozi wa timu hiyo Septemba 7,  2023 nchini Algeria, Katibu Mkuu Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo Saidi Yakubu ambaye aliongoza msafara wa timu hiyo, amewapongeza wachezaji na benchi la ufundi kwa kazi kubwa waliyofanya kwa kuwa safari ya matokeo hayo haikuwa nyepesi hadi dakika ya mwisho.

“Kwa niaba ya Serikali, Mhe. Rais, Mhe. Waziri pamoja na wadau wote, tumekuja hapa kuongeza hamasa. Kubwa mtakumbuka wakati wa kujiandaa na mechi ya Uganda kule nyumbani Mhe. Rais alitoa ahadi ya kutoa Shilingi milioni 500, timu ikifuzu. Nafurahi kuwaambia kwamba hizo fedha sio tu kwamba zitatolewa, zimekwisha letwa Wizarani kwa ajili yenu”, alisisitiza Katibu Mkuu. Yakubu.

Timu ya Tanzania, Taifa Stars imefuzu kucheza Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) baada ya kutoka suluhu tasa (0-0) na Algeria katika mchezo wa mwisho wa Kundi F uliochezwa katika Uwanja wa May 19, nchini Algeria.

Taifa Stars ikiwa na alama 8 imeungana na Algeria yenye alama 16 katika Kundi hilo kushiriki Mashindano ya AFCON yatakayofanyika Ivory Coast na kuziacha nje ya Mashindano hayo timu za Uganda waliomaliaza na alama 7 na Niger waliomaliza na alama 2 huku Tanzania ikishiriki Mashindano hayo kwa mara ya tatu kihistoria baada ya mwaka 1980 nchini Nigeria na 2019 nchini Misri.