Taifa Stars Yawa Moto Yaichapa Madagascar Kwa Mkapa
Timu ya Taifa Taifa Stars imefanikiwa kupata ushindi wa bao 3-2 kwa moja katika mchezo uliopigwa kwenye uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam na kujiwekea mazingira mazuri ya kukaa nafasi ya pili katika kundi J.
Katika mchezo huo uliopigwa Septemba 07 majira ya saa 10:00 jioni Stars ndiyo iliyokuwa ya kwanza kuandika mabao mawili ambapo bao la kwanza lilifungwa mnamo dakika ya kwanza tu ya mchezo kupitia Ersato Nyoni aliyekwenda kupiga mkwaju wa penati kabla ya Novatus Dismas kwenda kupachika bao la pili.
Kabla shangwe na ndelemo hazijamalizika Madagascar nao walitoka nyuma na kusawazisha mabao yote mawili ndani ya kipindi hicho cha kwanza, ambapo bao la kwanza la Madagascar lilipachikwa na mchezaji jezi namba 10 aitwae Rakoto Marimalala Njiva aliyetokea benchi huku bao la pili likifungwa kwa mpira wa kufa uliokwenda kupigwa na mchezaji Fontaine Thomas jezi namba (21) mnamo dakika ya 45 kipindi cha kwanza; matokeo hayo yalibakia hivyo mpaka timu zinakwenda kwenye mapumziko.
Kipindi cha pili kilianza kwa kasi kama ilivyokuwa katika kipindi cha kwanza ambapo kabla Madagascar hawajajipanga sawasawa Taifa Stars ilirudi kambani kwa mara nyingine ambapo Feisal Salum (Fei Toto) alifanikiwa kupachika bao la tatu, akimalizia pasi safi kutoka kwa mchezaji wa kimataifa na nahodha wa timu hiyo ya Stars Mbwana Ally Samatta jezi namba(10).
Kocha wa Taifa Stars Kim Poulsen baada ya mchezo huo alisema kuwa anakipongeza kikosi chake kwa kujituma na kuweza kupata matokeo hayo ambayo ni mtaji mzuri kwa safari ya kusaka tiketi ya kwenda kucheza Kombe la Dunia huko Qutar, licha ya kuruhusu mabao mawili katika kipindi cha kwanza. Hata hivyo, kocha Kim alisema kuwa mchezo huo umekwisha sasa kilicho mbele yake ni kujiandaa vema kwenye mchezo utakaofuata na Benin huku akijipanga zaidi kwa michezo iliyobaki.
Kocha Kim aliongeza kuwa lengo lake kubwa ni kushinda kila mchezo pasipo kujali kuwa nyumbani au ugenini; alisema kuwa kwake yeye mchezaji atakayeonesha uwezo na kujituma zaidi ndiye atakayepewa nafasi ya kucheza na sio ukubwa wa jina la mchezaji wala klabu anayochezea.
Kwa upande wa kocha wa Erick Sandratana, yeye alidai kuwa kikosi chake kimepoteza mchezo huo wa pili kutokana na makosa ya kiufundi yaliyofanyika kwenye kipindi cha pili licha ya kufanya vema katika kipindi cha kwanza ambapo waliweza kukomboa magoli mawili. Kocha huyo alieleza kuwa watazidi kuyafanyia kazi makosa ili waweze pata matokeo kwenye michezo mingine iliyosalia.
Kwa ushindi huo, Taifa Stars na Benin sasa wanafungana alama, wakiwa kwenye nafasi ya kwanza katika kundi “J” huku nafasi inayofutia ikishikwa na Congo DR baada ya timu zote wakati Madagascar wao wakiburuza Mkia.