Tambo za makocha kuelekea nusu fainali ya ligi ya vijana U-20

Michezo miwili ya nusu fainali ya ligi kuu ya vijana chini ya umri wa miaka 20 kupigwa Julai 15,2022 katika dimba la Azam Complex Chamazi, michezo hiyo itawakutanisha mabigwa watetezi Mtibwa sukari dhidi ya Azam Fc majira ya 9:00 Alasiri, ikifuatiwa na mchezo kati ya wagosi wa kaya Coastal Union wakikutana na Mbeya Kwanza majira ya saa 12:00 jioni.

Mbeya kwanza imetinga hatua hiyo ya nusu fainali baada ya kuitoa Yanga kwa kuichapa goli 1-0, goli pekee la Ahmed Hassan dakika ya 51. Mtibwa sukari ametinga hatua hiyo baada ya kuitupa nje Geita Gold kwa penalty 4-2 baada ya sare ya 1-1. Coastal union wakiiadhibu Simba sc kwa kuilaza goli moja bila majibu, goli lililopatokana dk ya 48 ya mchezo, na wenyeji Azam Fc wao wakiwafungashia virago Polisi Tanzania kwa ushindi wa penalty 6-5 baada ya sare ya 1-1.

Tambo za makocha wa timu zote zilizoingia nusu fainali zimeendelee kuelekea katika michezo hiyo, kocha wa Mtibwa sukari Awadh Juma alisema “ligi ya mwaka huu imekuwa na ushindani wa hali ya juu ukilinganisha na misimu iliyopita, Mtibwa kukutana na Azam sio mara ya kwanza hata mwaka jana tuliwatoa katika hatua hii na wanafahamu makali yetu hivyo tunakwenda kulinda heshima yetu tukitaka kombe kwa mara nyingine tena”.

Naye kocha wa Azam Fc John Matambala amesema mchezo utakuwa mgumu na mzito sana, kikubwa ni wao kwenda kujiandaa vizuri na kurekebisha makosa yaliyotokea katika mechi za nyuma, ubora wa Mtibwa wanaujua hivyo wamejipanga kuwakabilii na wanawakumbusha Mtibwa Sugar kuwa Azam complex ni uwanja wa nyumbani na wana uzoefu nao.

Mchezo wa mwisho katika hatua ya nusu fainali utawakutanisha Kocha wa Coastal Union dhidi ya Mbeya kwanza ambapo kocha wa Coastal Union Shabani Bakari alisema wamejiandaa vizuri kukabiliana na kila mpinzani kwasababu walishajiandaa kwa ajili ya mashindano hayo na wanaamini watakwenda kufanya vizuri huku wakiwaahidi wakazi wa Tanga kurudi na kombe nyumbani na waendelee kuwaamini na kuwaunga mkono.

Kocha wa Mbeya kwanza Baraka Kibanga alisema “Coastal Union ni timu nzuri sana walicheza vizuri sana katika mchezo wa robo fainali na kiujumla kwa upande wangu ni timu bora katika mashindano lakini licha ya ubora wao na sisi tumejiandaa kwa kiwango hicho hicho na kuingia katika hatua ya fainali ni moja ya malengo yetu ambayo tunakwenda kuyatimiza kesho”.