Kim; Tanzania Bado Inanafasi ya Kufanya Vizuri AFCON

Kocha Mkuu wa kikosi cha “Taifa Stars” Kim Poulsen amesema kuwa Tanzania bado inanafasi ya kufanya vyema katika kusaka tiketi ya kufuzu kushiriki AFCON mwaka 2023.

Hayo aliyasema Juni 8, 2022 mara baada ya timu hiyo ya taifa ya Tanzania kulazimishwa kuachia alama tatu ikiwa nyumbani kwa kuruhusu kufungwa mabao 2-0 katika mchezo wake wa pili dhidi ya Algeria uliopigwa majira ya saa 1:00 usiku kwenye uwanja wa Mkapa uliopo Jijini Dar es Salaam.

Akielezea kuhusu kiwango cha ‘Stars’ kilichooneshwa katika mchezo huo dhidi ya Algeria, kocha Kim alisema kikosi chake kilipambana kiume kuhakikisha kinaizuia timu hiyo ili kuweza kupata alama yeyote lakini ubora na uzoefu wa wapinzani wao ndio uliokwenda kuamua matokeo ya mchezo huo.

Aidha, kocha Kim aliongeza kuwa timu ya Algeria ni miongoni mwa timu bora Barani Afrika zenye viwango vya juu ukilinganisha na kikosi cha Tanzania ambacho kinaundwa na wachezaji wenye viwango vya wastani huku wengi wao wakiwa ni wachezaji wa ndani na wachache ndio wanaocheza mpira wa kulipwa ughaibuni.

Akifafanua kuhusu uwezekanao wa Tanzania kuweza kufuzu katika michuano hiyo mikubwa Afrika, Kim alisema anaamini michezo itakayochezwa mwaka huu ya michuano ya CHAN itakuwa ni sehemu moja wapo ya kuimarisha kikosi huku ikiliwezesha benchi la ufundi kurekebisha makosa yaliyojitokeza kwani watapata muda mrefu wa kukaa na wachezaji wengi kwa kuwa ligi zitakuwa zimesimama na kutoa nafasi ya kujumuika pamoja.

Mchezo huo kati ya Tanzania na Algeria ulimalizika kwa timu ya Tanzania kupoteza na kusalia na alama moja iliyoipata katika mchezo wa awali ulichezwa dhidi ya Niger Juni 4, mwaka huu nchini Benini ambapo “Taifa Stars” ilifanikiwa kuvuna alama hiyo moja sawa na Uganda ambayo nayo ilishindwa kutamba nyumbani kwenye mchezo wake dhidi ya Niger uliopigwa mapema kabla ya mchezo wa Stars na wa Algeria.

Matokeo ya michezo ya Juni 8, 2022 ya kundi F yalibadili msimamo wa kundi hilo ambapo kundi linaongozwa na Algeria aliyejikusanyia alama zote 6 baada ya kucheza na kushinda michezo miwili, akifuatiwa na Niger mwenye alama 2 baada ya kutoka sare ya bao1-1 katika mechi zote mbili nyumbani na ugenini, kisha inafuata Tanzania yenye alama moja iliyoipata ugenini dhai ya Niger huku Uganda yenyewe ikisalia mwisho baada ya kupata alama 1 katika mchezo wake wa nyumbani.