Tanzania bingwa CECAFA -U-18 2023

Timu ya taifa ya wanawake wenye umri chini ya miaka 18 imefanikiwa kutwaa ubingwa wa CECAFA U-18 baada ya kuifunga timu ya Uganda goli 1-0 katika mchezo wa mwisho wa kuhitimisha mashindano hayo uliochezwa katika uwanja wa Azam Complex Chamazi, Dar es Salam.

Mchezo huo ulionekana kuwa mgumu tangu dakika ya mwanzo hadi ya mwisho kwani licha ya timu ya Tanzania kupata goli dakika ya 43 kupitia kwa Winifrida Gerald bado timu ya Uganda iliendelea kulisakama lango la Tanzania.

Kocha mkuu wa timu ya Tanzania U-18 Bakari Shime aliwapongeza wachezaji wake kwa kucheza vizuri katika mashindano hayo pasipo kupoteza mchezo wowote lakini pia kwa kuonyesha ushindani na ukomavu wa hali ya juu.

” Kutwaa ubingwa wa CECAFA U-18 ni ishara nzuri kwamba tupo katika njia sahihi ya kukuza na kuendeleza vipaji vya vijana lakini pia ni mwanzo mzuri wa kuendelea kutwaa ubingwa  wa mashindano mengine yaliyo mbele yetu” alisema Kocha Shime.

Tuzo mbalimbali zilitolewa  baada ya mchezo huo kumalizika ikiwemo tuzo ya mchezaji bora iliyoenda kwa mchezaji Winifrida Gerald (Tanzania), Golikipa Bora ilichukuliwa na Husna Mtunda ( Tanzania), mfungaji Bora ilibebwa na Emush Daniel Dandamo (Ethiopia) huku timu ya Burundi ikinyakua Tuzo ya’ Fair play’.

Timu ya Uganda ilimaliza katika nafasi ya pili na Ethiopia akimaliza nafasi ya tatu, tuzo nyingine za heshima kwa watu wenye mchango mkubwa katika kukuza na kuendeleza soka la wanawake zilienda kwa kocha mkuu wa timu ya Taifa ya Wanawake Bakari Shime pamoja na Brigedia Jenerali Hassan Rashid Mabena ambaye ni Mkuu wa Tawi la utawala makao makuu JKT.

Mashindano ya CECAFA U-18 yalianza Julai 25,2023 yakijumuisha nchi 5 kutoka ukanda wa CECAFA ambazo ni Ethiopia, Burundi, Uganda, Zanzibar pamoja na mwenyeji Tanzania.